HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kupitia fedha za kuwajengea uwezo watumishi (ULGSP) imetoa mafunzo kwa walimu 50 wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule za msingi na sekondari.
Mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa siku moja kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea,yamefunguliwa na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema.
Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo hayo,Mgema amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa walimu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa aina mbalimbali wakiwemo wanafunzi wasioona,wasiosikia,wenye ulemavu wa akili na wenye ulemavu zaidi ya mmoja ili walimu waweze kutoa elimu kwa ufanisi.
Amesema serikali kwa kutambua uwepo wa wanafunzi wenye mahitaji maalum,imeweka mazingira ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanapata elimu sawa,ndiyo maana serikali imeanzishwa vyuo vya elimu maalum.
“Nawapongeza kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya,lakini natambua kuwa tuna upungufu mkubwa wa walimu wa elimu maalum ambao wanaweza kuwasaidia vijana wetu wenye mahitaji maalum ’’,alisema Mgema.
Kwa mujibu wa Mgema,mafunzo hayo yatawawezesha walimu ambao hawakupata mafunzo maalum,kuweza kutambua mambo muhimu kama lugha za alama na maandishi ya nukta nundu ili waweze kusaidia kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake Afisa Elimu maalum katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Rehema Nyagawa amesema katika Manispaa hiyo kuna jumla ya wanafunzi 405 wenye mahitaji maalum kati yao wavulana 243 na wasichana 162.
Nyagawa amesema Manispaa ya Songea ina jumla ya walimu 52 tu waliosomea kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum na kwamba kuna walimu 12 ambao wanafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum bila kusomea elimu maalum.
“Manispaa ya Songea ina upungufu wa walimu wenye mahitaji maalum 13,walimu waliopo ni 52,jumla ya walimu 65 wanahitajika,hivyo kutokana na upungufu uliopo,ni vema kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa walimu wasiokuwa na mafunzo maalum’’,alisema Nyagawa.
Akizungumza wakati anafunga mafunzo hayo,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Tina Sekambo amewapongeza walimu wanaofundisha watoto wenye mahitaji maalum na kusisitiza kuwa serikali inatambua kazi ngumu wanayoifanya hivyo wasikate tamaa bali waendelee kuchapakazi.
“Kazi mnayoifanya ni ngumu sana ,iwapo mwalimu anayefundisha wanafunzi wasiokuwa na ulemavu anapata tabu,je ninyi wenye ulemavu….hatuna cha kuwalipa,bali anayeweza kuwalipa ni Mwenyezi Mungu pekee’’,anasisitiza Sekambo.
Manispaa ya Songea ina vitengo tisa ambavyo vinafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum na shule moja maalum ya bweni ya Mtakatifu Vincent inayofundisha wanafunzi viziwi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Novemba Mosi,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa