HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea imeanza rasmi upuliziaji mazalia ya mbu katika mitaa 95 iliyopo kwenye kata 21 zilizopo katika Halmashauri hiyo.Afisa Afya Mkuu wa Manispaa ya Songea Vitalis Mkomela amesema zoezi la upuliziaji limeanza Oktoba 19 mwaka huu katika mitaa ya kata za Bombambili, Mfaranyaki, Matarawe na Mjini.
Amesema zoezi limefanyika katika mazalio ya wazi ambayo mbu wa malaria hutaga mayai na kuzalisha mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria.Kwa mujibu wa Afisa Afya huyo hadi sasa jumla ya mazalio ya maji 212 na mabwawa manane yamepuliziwa dawa na kwamba zoezi hilo linafanyika kata hadi kata.Hata hivyo anazitaja changamoto ambazo zimejitokeza hadi sasa ni zoezi hilo Kutokuwa kwenye mpango wa Halmashauri hivyo kukosa fedha za kununua vifaa na kuwalipa wapuliziaji hali ambayo imesababisha zoezi hilo kuanza katika mitaa 49 iliyopo katika kata kumi kati ya mitaa 95 iliyopo katika kata 21.
Changamoto nyingine anaitaja kuwa ni Kukosekana kwa maafisa afya katika kata nane,ambao ni wataalam wa zoezi hili katika kata zao.Anaitaja mikakati ambayo inachukuliwa ili kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni Kuandaa bajeti ya upuliziaji na kuingiza katika mpango wa mwaka 2018/ 2019.Kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi la upuliziaji,Halmashauri ya Manispaa ya Songea ilianza kutekeleza zoezi la upuliziaji kwa kufanya mkutano elekezi kwa wenyeviti na Maafisa watendaji wa mitaa 49 ambayo ipo katika kata kumi.
Mkutano huo ulijadili masuala muhimu ya zoezi la kuua viluwiluwi wa mbu,kuhamasisha wananchi Kutambua mazalio ya mbu katika maeneo yao na namna ya kumteuwa mpuliziaji wa viuadudu wa kujitolea kutoka katika mitaa yao.Baada ya mkutano huo wenyeviti wa mitaa na maafisa watendaji waliteua mpuliziaji kutoka katika kila mtaa ambao walifanyiwa mafunzo namna ya kupulizia viuadudu katika mazalio ya wazi na mazalio yaliyofunikwa.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa