HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imesaini Mkataba wa ukusanyaji wa ushuru wa mazao wa shilingi milioni 610 na kampuni ya WOFMAIZE ya Songea.
Makubaliano ya kusaini Mkataba huo yamekamilika Oktoba 24 mwaka huu katika Ofisi ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji, yakishuhudiwa na wawakilishi wa Kampuni ya WOFMAIZE pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Eng.Samwel Sanya.Kampuni hiyo itahusika na ushuru wa mazao ya vyakula vilivyosindikwa na visivyosindikwa katika maeneo ya SODECO,Manzese na maeneo mengine ya Manispaa ya Songea.
Mkataba huo ni wa miezi tisa ambao unaanza Oktoba 2017 hadi Juni 30,2018 ambapo kampuni ya WOFMAIZE italipwa asilimia 15 ya makusanyo yote katika kipindi hicho ambayo ni sawa na zaidi ya milioni 90.Akizungumza mara baada ya kusaini Mkataba huo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea ameipongeza kampuni hiyo kwa kushinda zabuni ya ukusanyaji ushuru ambapo ameitaka Kampuni kukusanya ushuru kwa uaminifu kwa kuwa Manispaa ya Songea bado inategemea kupata mapato kupitia ushuru wa mazao.
Mkurugenzi wa WOFMAIZE Wofram Mlowe ameahidi Kampuni yake kufanyakazi kwa uaminifu mkubwa ili kufikia malengo ya kukusanya milioni 610 au zaidi katika kipindi cha miezi tisa.Manispaa ya Songea imeamua kusaini makubaliano ya mkataba kwa ajili ya ubinafsishaji wa vyanzo vya mapato katika kipindi cha mwaka 2017/2018 lengo likiwa kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 100.
Taarifa Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa