HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imetoa jumla ya sh.milioni 45 kwa ajili ya kutoa mikopo katika vikundi 49 vya wajasirimali wadogo.Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo Naftari Saiyoloi ametoa taarifa hiyo katika uzinduzi wa mfuko wa vijana na wanawake kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Amebainisha kuwa sh.milioni tisa zitakopeshwa kwa vikundi kumi vya vijana na sh.milioni 36 zitakopeshwa vikundi 39 vya wanawake.Saiyoloi amebainisha kuwa kuanzia mwaka wa fedha wa 2014/2015 hadi mwaka wa fedha wa 2017/2018 Manispaa ya Songea imetoa zaidi ya sh.milioni 181 kwenye mfuko wa wanawake na vijana.Hata hivyo amesema kati ya fedha hizo,sh.milioni 116 zinatokana na mapato ya ndani na zaidi ya milioni 65 zinatokana na marejesho yaliofanyika kutokana na vikundi vinavyokopeshwa na kurejesha mkopo.
“Idadi ya vikundi vya wanawake vilivyonufaika kwa fedha hizi ni 202 na kiasi kilichokopeshwa ni zaidi ya milioni 126,idadi ya vikundi 115 vya vijana vilinufaika na mkopo wa zaidi milioni 55’’,alisema Saiyoloi.Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo huyo,Manispaa ya Songea katika kipindi hicho ilitoa jumla ya sh.milioni 92 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana.
Amesema kati ya fedha hizo milioni 3.2 zilitumika kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji na milioni 88.8 vilikopeshwa vikundi vya wanawake 77 kiasi cha sh.milioni 59.8 na vikundi vya vijana 56 vilikopeshwa milioni 29.Amebainisha kuwa fedha za vikundi vya wanawake zilizorejeshwa ni zaidi ya milioni 53 na fedha za vikundi vya vijana zilizorejeshwa ni zaidi ya milioni tisa.
Mgeni rasmi katika utoaji wa mikopo hiyo,Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Leonidas Gama ameipongeza Manispaa ya Songea kwa kutoa kwa wakati asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya kukopesha vijana na wanawake.Amesema mikopo hiyo ni muhimu kwa wanawake na vijana kwa sababu umasikini mkubwa upo katika ngazi ya familia ambapo mkopo huo unachangia kupunguza umaskini kwa wanyonge.
Taarifa imetolewa na
Albano Midelo Afisa Habari wa Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa