MAONESHO ya viwanda na uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma yanatarajia kufanyika kwa siku tatu katika uwanja wa Majimaji mjini Songea kuanzia Julai 24 hadi 26 mwaka huu.
Akizungumza katika kikao cha maandalizi ya tamasha hilo ngazi ya Wilaya ya Songea kilichofanyika kwenye ukumbi wa Songea Klabu,Mkuu wa Wilaya hiyo Pololet Mgema amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ambaye anatarajia kuzindua tamasha hilo Julai 25 mwaka huu.
Amesema Waziri Mkuu anatarajia kuzindua Mwongozo wa uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma ambao umeandaliwa na wasomi ukionesha furs azote za uwekezaji na utalii zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma na kwamba baada ya uzinduzi huo Mwongozo utasambazwa ndani nan je ya nchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kihabari ili kuzitangaza fursa hizo kitaifa na kimataifa.
“Mkoa wa Ruvuma umekusudia kufanya maonesho ya viwanda na uwekezeshaji ili kuuweka Mkoa katika Ramani ya fursa mbalimbali za viwanda,uwekezaji na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma’’,alisisitiza Mgema.
Amesema serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekusudia kufungua milango ya uwekezaji na kutangaza fursa za utalii katika mikao saba ya kusini ambayo ni Ruvuma, Rukwa, Songwe,Katavi,Mbeya,Njombe na Iringa.
Kulingana na Mkuu huyo wa Wilaya Kongamano hilo la viwanda na uwekezaji litashirikisha Kampuni mbalimbali,Taasisi na wajasirimali wengine kutangaza shughuli zao hivyo kusababisha wawekezaji wengi ndani na nje ya nchi kuwekeza katika Mkoa wa Ruvuma.
Ametoa rai kwa Halmashauri zote mkoani Ruvuma kutumia maonesha hayo kubainisha maeneo ya viwanda,uwekezaji na utalii ili yafahamike na wawekezaji waweze kufika na kuwekeza hali ambayo itakuza uchumi na kuongeza ajira kwa vijana.
“Serikali ya Awamu ya tano imejitahidi kuboresha miundombinu ya barabara,viwanja vya ndege na majini hivyo ni vema sasa kuzitangaza furs azote zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma ili kuwakaribisha wawekezaji.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini Manispaa ya Songea
Julai 15,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa