TUKIWA katika maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani ambayo inaanza Mei 31 na kilele chake Juni 5 kila mwaka,kauli mbiu ya mwaka huu inasema matumizi ya mkaa ni gharama,tutumie njia mbadala.
Katika tafiti zilizofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN HABITAT) mwaka 2008 zimeonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinaongoza kwa matumizi ya nishati ya mkaa.
Utafiti wa kimataifa unaonesha kuwa watu bilioni tatu duniani kati ya bilioni saba wanatumia mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia na shughuli nyingine zinazohitaji nishati ya mkaa na kuni hali ambayo inaiweka Dunia njia panda katika suala la kuzuia uteketezaji wa misitu.
Hii ina maana ya kwamba uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa miti holela ni mkubwa na unahitaji nguvu ya ziada kwa wadau kutoka ngazi zote kuanzia familia,Kitongoji,Mtaa Kijiji,Kata,Tarafa,Wilaya ,Mkoa,Taifa na kimataifa kwa ujumla ili kurekebisha na kurudisha miti inayokatwa kwa ajili ya uchomaji mkaa na kuni.
Mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini na duniani kote kwa ujumla ni dalili kuwa binadamu wamefanya uharibifu mkubwa wa mazingira yanayowazunguka hasa vitendo vya ukataji wa miti hovyo.
Takwimu zinaonesha kuwaTanzania inapoteza kiasi cha hekta 400,000 za misitu kila mwaka kwa sababu ya ukataji miti unaochochewa na matumizi ya kuni, mkaa, mbao, ujenzi ama uchomaji moto misitu.Matumizi ya mkaa mijini ni makubwa kuliko vijijini wakati matumizi ya kuni vijijini ni makubwa kuliko mijini.
Waziri Mstaafu wa Maliasili na Utalii Prof.Jumanne Maghembe anasisitiza kuwa moja ya vitu ambavyo vinaongoza kwa kuteketeza misitu ni biashara ya mkaa ambapo anashauri mikoa michache ambayo hakuna ukataji mkaa wa kutisha kama Mkoa wa Ruvuma,waanze kutumia sheria ndogo ndogo ili kukabiliana na watu wanaofanyabiashara hiyo ambayo imesababisha asilimia 60 ya Tanzania kuathirika na jangwa.
”Nani amemuona mtu anayekata miti na kufanya biashara ya mkaa amekuwa tajiri,utamuona ana majivu tu kila siku, kwa sababu miti hii ni viumbe hai na wanaoikata wanafanya dhambi kubwa sana kwa Mwenyezi Mungu’’,anasema Prof.Maghembe
Utafiti uliofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Services (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mradi wake wa tathmini ya rasilimali za misitu Nchi unaonesha kuwa ukataji huo wa misitu unasababishwa kuzalishwa kwa zaidi ya tani milioni moja za mkaa kila mwaka ambao nusu yake yaani tani 500,000 unatumiwa na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam pekee.
Dk. Felician Kilahama ni Mkurugenzi Mstaafu, Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii anasema teknolojia inayotumika kutengeneza mkaa inasababisha kupatikana mkaa kidogo wakati miti mingi imetumika. Kwa mfano, mtegeneza mkaa kwa kutumia tanuru la udongo hupata tani moja ya mkaa kwa kutumia tani 10 hadi 12 za miti iliyokatwa.
Dk.Kilahama anaishauri Serikali kutafuta njia mbadala ya kupikia kwa kutumia gesi kama LPG (Liquefied Petroleum Gas) au hata gesi asilia (Natural Gas) pamoja na vyanzo vingine kama kutumia umeme badala ya mkaa.
Kutokana na misitu tunapata dawa za asili ambapo utafiti unaonesha kuwa asilimia 75 ya dawa za hospitali vyanzo vyake ni misitu ya asili na mimea mbalimbali. Kwa hiyo jitihada zifanyike ili kuinusuru misitu ya asili isiendelee kuangamia kwa mahitaji makubwa ya mkaa.
Makala haya yameandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 3,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa