NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
15.10.2021
Wananchi wa Manispaa ya Songea wampongeza Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Dr. Damas Ndumbaro kwa kufadhili huduma ya upimaji wa afya ya macho bure, zoezi ambalo limeanza kufanyika leo tarehe 15 hadi 17 Oktoba 2021 katika eneo la bustani ya Manispaa ya Songea kwa lengo la kusheherekea maadhimisho ya siku ya afya ya macho duniani.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano amewashukuru wataalamu wa afya ya macho kutoka katika Hospitali ya St. Joseph Peramiho kwa kukubali kufanya zoezi la kutoa elimu juu ya afya ya macho na jinsi ya kutunza na kuzuia upofu wa macho pamoja na uchunguzi wa macho kwa wananchi wote waliopo ndani ya Manispaa ya Songea.
Mbano ametoa wito kwa wananchi wote kutumia fursa hii kwa kujitokeza kwa wingi ili kupima afya ya macho, huduma ambayo inatolewa bure kwa udhamini wa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini.
Kwa upande wake Katibu wa Mbunge Jimbo la Songea Mjini Joel Alex Ndunguru, amesema lengo la Mbunge kufadhili zoezi la upimaji wa afya ya macho kwa Wananchi ni kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa ya watu wenye matatizo ya macho wanaohitaji msaada kutoka katika ofisi yake na hiyo ikapelekea kuwaomba wataalamu wa afya ya macho kutoka Hospitali ya St Joseph Peramiho kuwapima wananchi wake bure pamoja na kutoa huduma ya dawa na miwani kwa gharama nafuu.
Nae Mtaalamu wa afya ya macho Dr. Goodlove Kyando amesema kuwa zoezi hili ni la muda wa siku tatu kuanzia leo hadi tarehe 17 Oktoba 2021, na hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi ili waweze kujua afya ya macho hasa ugonjwa wa presha ya macho ambao hauwezi kujulikana hadi upate vipimo sahihi kutoka kwa wataalamu wa afya ya macho.
Amesema kuwa watoto wamepewa kipaumbele kikubwa katika zoezi hilo ambapo amewasisitiza wazazi na walezi kuwaleta watoto wao ili waweze kupimwa na kupatiwa matibabu bure kabisa ikiwemo dawa, miwani na operesheni pale inapohitajikaa.”Kyando Alisisitiza”
Wananchi na viongozi mbalimbali ikiwemo na Madiwani wa Manispaa ya Songea wamejitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la upimaji wa afya ya macho na wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini kwa kufadhili zoezi hilo pamoja na kupongeza huduma nzuri ya upimaji wa macho inayotolewa na wataalamu wa afya ya macho kutoka St Joseph Mission Hospital Peramiho.
Kauli mbiu ya siku ya macho duniani ni; ‘YAPENDE MACHO YAKO, NENDA KAPIME SASA, KILA MTU ANAHUSIKA’
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa