Na;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
29.12.2021
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefanya tahimini ya mkakati wa uboreshaji wa Elimu ya ufaulu katika sekta ya elimu msingi na sekondari kwa mwaka 2022.
Tathimini hiyo imefanyika leo tarehe 29 Desemba 2021 katika ukumbi wa shule ya wasichana (Songea girls) Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii (Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini) Dkt. Damas Ndumbaro, Waheshimiwa Madiwani, wakuu wa shule za Msingi na Sekondari, wadau wa elimu pamoja na viongozi mbalimbali kutoka ndani ya Manispaa ya Songea.
Akizungumza katika tathimini hiyo Mgeni rasmi Dkt. Damas Ndumbaro amewataka walimu kuhakikisha wanazingatia miiko ya taaluma yao pamoja na kuhakikisha wanajiendeleza kielimu kwa lengo la kuboresha sekta ya elimu nchini na kutoa elimu bora kwa wanafunzi.
Dkt. Ndumbaro ametoa wito kwa walimu kuzingatia uwepo wa michezo mashuleni kwa kuandaa bonanza mbalimbali kwa lengo la kuimarisha afya ya mwili na akili ya wanafunzi ambapo amehaidi kutoa vifaa vya michezo kwa kwa shule ambazo zitakuwa tayari kushiriki katika matamasha mbalimbali ya michezo.’Alisisitiza’
Amewapongeza walimu wa Manispaa ya Songea kwa kuendelea kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita ambapo alitoa zawadi kwa walimu waliofanya vizuri zaidi kwa somo la Hisabati ambapo walimu waliopokea zawadi hizo kutoka shule mbalimbali ikiwemo na shule ya wavulana Songea (Songea Boys), shule ya wasichana Songea (Songea Girls), shule ya Sekondari Matarawe, shule ya Sekondari Msamala, shule ya sekondari Ruvuma pamoja na shule ya sekondari Bombambili,n.k
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanachangia mchango wa chakula kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni ikiwa ni miongoni mwa mikakati itakayosaidia kuongeza uboreshaji wa ufaulu kwa wanafunzi.
Dkt. Sagamiko aliongeza kuwa sababu ya kuwepo kwa tathimini ya mpango shirikishi wa elimu ni kuhakikisha mikakati iliyowekwa inafanyika kwa kushirikiana kwa pamoja ili kuleta tija na mabadiliko katika Nyanja ya elimu ndani ya Manispaa ya Songea kwa mwaka 2022.
Amewataka walimu, Maafisa elimu kata pamoja na watendaji kata kuhakikisha wanawajibika katika nafasi zao ili kuweza kutekeleza mikakati iliyowekwa kwa kila mmoja asimame kwenye majukumu aliyopangiwa.
Akibainisha mikakati iliyowekwa ya uboreshaji ufaulu katika sekta ya elimu msingi na sekondari kwa mwaka 2022, Afisa elimu Sekondari Manispaa ya Songea Devotha Luwungo alisema kuwa lengo kuu la mkakati huo ni kutumia rasilimali watu na fedha ili kufikia ufaulu wa asilimia 98% hadi 100% kwa shule za msingi, ufaulu wa daraja la I hadi III kwa kidato cha nne pamoja na daraja la I hadi II kwa kidato cha sita.
Alisema kuwa ili kufikia kiwango cha ufaulu wa asilimi 98%-100% Manispaa ya Songea imejipanga kuhakikisha muhtasari (syllabus) zinakamilishwa ifikapo mwezi wa 5 kwa shule za msingi na mwezi wa 6 kwa shule za sekondari ili kutoa nafasi ya wanafunzi kufanya marudio pamoja na uboresahji wa mbinu za ufundishaji ikiwemo na ufundishaji kwa njia ya majadiliano, ziara za moasomo pamoja na matumizi ya zana za kufundishia.”Alibainisha”
Akieleza majukumu ya wadau mbalimbali wa elimu Afisa elimu Msingi na Awali Frank Sichalwe alisema kuwa kila mdau wa elimu katika nafasi yake anatakiwa kuhamasisha wazazi kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo na kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule pamoja na kuhamasisha jamii kutoa ushirikiano katika kudhibiti utoro kwa wanafunzi kwa lengo la kuboresha kiwango cha ufaulu mashuleni.
Akisisitiza ushirikiano kati ya walimu na viongozi wa Serikali za mitaa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano amewataka wakuu wa shule na viongozi wa bodi za shule kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na Madiwani kwa lengo la kutekeleza mikakati iliyowekwa kwa pamoja.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina jumla ya shule ina jumla za Msingi 94 ambapo shule 80 ni za Serikali na 14 ni shule za binafsi zenye idadi ya wanafunzi wa shule za Serikali ni 55,548 ( Wav 27609, Was 27939) na shule binafsi ni 4,1969 (Wav 1,877 na Was 2319).
Kwa upande wa Elimu Sekondari ina jumla ya shule 42, kati ya hizo 24 ni shule za Serikali na 18 ni shule binafsi ambapo hadi kufikia mwezi 2021 katika shule za Serikali ina jumla ya wanafunzi 16817 ikiwa na wavulana 7919 na wasichana 8900 pia katika shule binafsi zina jumla ya wanafunzi 2823 kwa wavulana 1519 na wasichana 1304.
Wadau walioshiriki kikao hicho, walitoa maoni yao kwa pamoja na walikubali kupitisha mkakati wa kuboresha elimu ambapo amewataka walimu wote Manispaa ya Songea kupokea na kutekeleza mkakati huo ili uweze kuleta tija katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Mwisho
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa