Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
17 JUNI 2022
Kila mwaka tarehe 16 Juni Tanzania inaungana na nchi zingine za Afrika kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika.
Chimbuko la maadhimisho haya ni azimio lililopitishwa na Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika kusini waliouawa tarehe 16 Juni 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Katika Manispaa ya Songea Maadhimisho hayo yamefanyika jana Juni 16, 2022 katika viwanja vya Zimanimoto na kuhudhuriwa na wananchi mbalimbali, viongozi, walimu, wadau mbalimbali pamoja na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zilizopo ndani ya Manispaa ya Songea.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano alisema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi hasa kupata elimu ambapo watoto wataendelea kusoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita kama ilivyoelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan.
Amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanazungumza na watoto ili kubaini changamoto mbalimbali wanazokutana nazo hasa vitendo hatarishi wanavyotendewa wanapokuwa nje na maeneo ya nyumbani.
Ametoa rai kwa walimu kuwa na mahusino ya karibu na watoto pamoja na kuwatunza ili kuimarisha ulinzi wa watoto wanapokuwa shuleni.
Mbano amaezitaka Taasisi zisizo za kiserikali zinazohusiana na utetezi wa haki za watoto kuendelea kutoa elimu ya malezi kwa jamii kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwemo na ubakaji, ulawiti pamoja na mimba za utotoni.”Alibainisha”
Alisema watoto wote kutoa taarifa juu ya ukatili unaofanywa na baadhi ya watu wasiona mapenzi mema, ambapo amewarai wanafunzi hao kutoa taarifa mapema kwa walimu, viongozi wa Serikali za mitaa pamoja na dawati la jinsia lililopo katika vituo vyote vya polisi, mara wanapoona kuna changamoto za zinazoashiria ukatili.
Pia, amewataka watoto kuwa mabalozi kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika ifikapo Agosti 23, 2022 nchini Tanzania.
Kwa upande wake Mratibu wa Maadhimisho hayo Joyce Mwanja (Afisa maendeleo ya jamii Manispaa ya Songea) alisema kuwa kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu ni “Tuimarishe ulinzi wa mtoto, tokomeza ukatili dhidi yake, jiandae kuhesabiwa” ambayo inakumbusha jamii juu ya wajibu wa kuimarisha ulinzi kwa watoto pamoja na kupinga vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watoto katika jamii.’Alisisitiza’
Mwanja alisema kuwa Manispaa ya Songea imetumia siku hiyo kwa kutoa elimu juu ya kupinga ukatili wa watoto, chanzo na madhara yake kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi sekondari.
Ametoa rai kwa vikundi mbalimbali vya wajasiriamali na vikoba kuweka ajenda ya kujadili malezi ya watoto katika jamii katika vikao vyao ambayo itawawezesha kuwapa elimu watoto juu ya namna ya kugundua mazingira hatarishi na namna ya kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa