MJUSI huyo alivumbuliwa katika eneo la Tendaguru wilayani Kilwa,mkoani Lindi miaka 100 iliyopita.Mjusi huyo ni kuvutio adimu katika makumbusho ya Berlin nchini Ujerumani ambaye ana uzito wa tani 50.Mjusi huyo kwa jina la kitaalam anaitwa dinosaurs ambapo masalia ya mjusi huyo toka katika eneo la Tendaguru,yalikusanywa na kupelekwa Ujerumani ambako watalaam waliyaunda na kisha kuyaweka kwenye Makumbusho ya Berlin yaliojengwa tangu mwaka 1889.
Tendaguru ndilo jina ambalo linatumiwa na watafiti na watalaam katika machapisho yaliopo kwenye makumbusho hayo ambapo wanalitumia jina hilo kutambulisha mijusi wote wakubwa sio wa Tanzania pekee bali pia wanaotoka katika nchi nyingine.Mjusi huyo anakadiriwa kuwa na umri wa miaka milioni 150,ana urefu wa meta 13.7 kwenda juu,anakadiriwa kuwa na moyo wenye uzito wa kilo 400 na chakula cha mjusi huyo kilikuwa ni mimea.
Mwanasayansi na Mtafiti wa Mambo ya kale Dk.Daniela Schliart anasema mjusi huyo aligundulika kati ya mwaka 1907 na 1909 ambapo watafiti katika eneo la Tendaguru walikuwa wanatafiti madini ndipo walikutana na masalio hayo kisha kukusanya masalia na kuyasafirisha hadi nchini Ujerumani.Wanasayansi hayo na watafiti walibaini kuwepo aina 13 tofauti za mijusi ambao baadhi yao waliishi kwa kula mimea na wengine nyama.
Mtafiti Dk.Daniella anabainisha namna walivyopata umri wa mjusi huyo ni kwa kuangalia makundi ya madini yalivyopangiliwa na kwa kutumia program za kompyuta.Masalio ya mjusi huyo yanatunzwa kwa kutumia kemikali maalum za kumlinda asijekusambaratika,na kwambaNaibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa kimataifa na Sayansi Dk.Christopher Hauser anasisitiza kuwa Tanzania inahitaji wataalam wa mambo kale ambao wamepata mafunzo maalum ya kuhudumia masalia ya mijusi wa kale.
“Tanzania itayarishe wataalam wa kutunza masalia ya mujusi kwa sababu imekaa miaka mingi hivyo inaweza kuharibika,utafiti unaonesha kuwa bado Tanzania kuna masalio ya mijusi katika eneo la Tendaguru na maeneo mengine’’,anasisitiza Dk.Hauser.
Licha ya kuhifadhiwa masalia ya mjusi huyo toka Tanzania,katika Makumbusho ya Ujerumani kuna masalia ya viumbe wengine ambao ni nyoka,ndege,simba,chui na mijusi wakubwa kutoka nchi mbalimbali.Makumbusho ya nchini Ujerumani yapo chini ya Wizara ya Elimu na Utafiti ambayo huingiza wastani wa watu 500,000 kwa mwaka ambapo kiingilio chake ni euro nane kwa kila mtu anayetembelea makumbusho hayo.
Mwandishi wa makala haya ni Albano Midelo mawasiliano yake albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa