MWANAFUNZI bora kitaifa katika matokeo ya mitihani ya kidato cha sita iliyofanyika mei mwaka huu, Anthony Mulokozi amesema, juhudi za kujisomea, kuwasikiliza walimu, ushirikiano na wenzake na kumuomba Mungu vimempa ushindi huo.
Kijana huyo aliyekuwa akisoma mchepuo wa PCB katika Sekondari ya Serikali ya Mzumbe iliyopo Morogoro ameyapokea matokeo hayo kwa shangwe kubwa.Antony ana ndoto ya kuwa daktari. Amesema akiwa nyumbani kwao Ngara mkoani Kagera kuwa, alipata taarifa za matokeo kutoka kwa kaka yake aliyemwambia matokeo yametoka, ampe namba yake ya mtihani.
Alisema baada ya kujua matokeo, alifurahi sana na kumshukuru Mungu, na kukimbilia shambani kumpa taarifa mzazi wake ambaye naye, alifurahi na wakaongozana kwenda internet café kuangalia hizo habari na kukuta amepata A zote.Hisia zake “Nilikuwa najua nitafanya vizuri, lakini sikutegemea kama nitakuja kuwa mwanafunzi bora kitaifa, ila nilijua nitafaulu vizuri,” alisema.
Alitaja siri ya mafanikio yake, kwanza ni kumuomba Mungu, kumtanguliza Mungu mbele lakini pia na kusoma sana.“Nilijitahidi kweli kusoma sana kwa kushirikiana na wenzangu, ndio kuna vitu vingine nilikuwa nafahamu na vingine sifahamu nilikuwa nauliza kwa wenzangu”.
Alisema siri nyingine ni kusikiliza walimu, “walimu wa Mzumbe kwa kweli walitutrain (kutufunza) vizuri jinsi ya kujibu maswali na kujiamini katika chumba cha mitihani, nawashukuru sana, lakini nilijitahidi sana kujipa muda wa kusoma, wakati wa likizo nilikuwa narudia pale nilipokuwa nashindwa shuleni, na siku nyingine nilikuwa nasoma zaidi ili walimu wakija kutufundisha nijue ni nini kinaendelea” alisema.
Amesema, alikuwa anafanya mazoezi ya kutosha huku akijitahidi kutafuta mitihani mingine, kuipitia na kuuliza wenzake na walimu. Ilikuwaje chumba cha mitihani?Anasema kwenye chumba cha mtihani alijitahidi sana kumtanguliza Mungu na kutulia: ”panic (hofu) ni mbaya sana, lakini niliamini nikisoma vizuri tu nitapata cha kujibu, kwa hiyo nilikuwa nikiona swali hili nalifahamu nilijitahidi kulijibu vizuri,”.
Pia alisema wazazi wake walijitahidi kumtia moyo, kwamba ajitahidi, ndugu zake pia walimtia moyo tangu mwanzo wakimwambia kwamba masomo ni magumu lakini akisoma vyema atashinda.
Ratiba ya kujisomea"Saa moja hadi saa nane tulikuwa na walimu na kuanzia saa 8:30 tulikuwa tunakwenda kula, halafu saa 9 mpaka saa 11:30, baada ya hapo nakwenda kuoga halafu saa moja nakwenda kipindi cha dini mpaka saa mbili, then prep nilikuwa nakwenda saa 2 mpaka saa 6:30 au saa saba hivi"amesema
CHANZO NI GAZETI LA SERIKALI LA JULAI 14,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa