Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
16.11.2021
Mganga mkuu Manispaa ya Songea Dkt. Amos Mwenda amewataka maafisa kilimo kutoa elimu ya kilimo cha mahindi lishe kwa wananchi na kamati za shule.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha lishe kilichofanyika hapo jana tarehe 15 Novemba 2021 kwa lengo la kufanya mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na kupanga bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Mwenda alisema katika kutekeleza afua za lishe Manispaa ya Songea imefikia hatua nzuri ukilinganisha na kipindi cha nyuma kwa kuzingatia viashiria vinavyotekeleza ambapo hali ya udumavu imefika asilimia 33.5%, hata hivyo elimu inaendelea kutolewa kwa jamii ili kuondoa hali ya utapiamlo mkali uliopo asilimia 0.1%.
Alisema Manispaa ya Songea imeweka mkakati wa kukabiliana na changamoto za afua za lishe ambazo ni pamoja na maafisa kilimo kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya mahindi lishe kwa wananchi na kamati za shule ili jamii iweze kupata uelewa wa kilimo cha mahindi lishe ambao utasidia wazabuni waweze kupata mahindi lishe ya kutosha na kupeleka mashuleni.
Aliongeza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea hutenga kwenye bajeti shilingi 1000 kwa kila mtoto ambapo katika mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Manispaa ya Songea imetenga shilingi 1900 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano.
Naye Afisa lishe Manispaa ya Songea Frolentine Kissaka amewataka wataalamu wa afya kuendelea kufanya ufuatiliaji, simamizi shirikishi pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu hao mahali pa kazi katika vituo vyote vvya kutolea huduma za afya na katika ngazi ya jamii.
Alieleza kuwa lishe ni pamoja na ulaji unaofaa ambao ni muhimu kwa afya ya lishe ya binadamu wote ambapo ulaji huo uzingatie ulaji wa chakula mchanganyiko na cha kutosha kinachopatikana kwa gharama nafuu katika mazingira yetu.
“Suala la lishe ni mtambuka siyo la idara ya afya pekee, kwahiyo sekta zote mtambuka zinajukumu la kupanga na kutekeleza afua za lishe ikiwa na lengo la kupambana na tatizo la utapiamlo kiwilaya” Kissaka alihitimisha.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa