9 Disemba ni siku ya Maadhimisho ya Uhuru Tanzania Bara ambayo huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kukumbuka historia ya harakati za uhuru wetu na kwa mchango wa viongozi wetu.
Awali Tanganyika ilijumuisha Rwanda na Burundi kuunda koloni la Mjerumani hadi mwaka 1914 ambapo ulikuwa mwisho wa vita vya kwanza vya dunia. Kuanzia tarehe 20 Julai, 1922 Tanganyika ilirasimishwa na kuwa chini ya mamlaka ya shirikisho la Mataifa (League of Nations) chini ya Uingereza.
Kwa upande wa Zanzibar, Historia inahusu eneo ambalo linaundwa na Jamhuri ya watu wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Eneo hili la Zanzibar lilipata uhuru kwa kufanya mapinduzi dhidi ya utawala wa Sultani na kuweka uongozi wa waafrika chini ya Chama cha ASP mwaka 1964 kilichoongozwa na Sheikh Abeid Amani Karume na ilipofika tarehe 26 Aprili, 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Baada ya Uhuru Tanganyika ilishuhudia mabadiliko mengi ya kisiasa ikiwa ni katika juhudi za kujipatia maendeleo na kuondoa mabaki ya utawala wa mkoloni ambapo viongozi wa Tanganyika waliunda Katiba iliyojikita kwenye mahitaji ya nchi mpya ambayo yalilenga mgawanyo wa mamlaka ya kisiasa na majukumu mbalimbali ya viongozi pamoja na wananchi.
Katika kuadhimisha Sherehe hii Manispaa ya Songea imeweza kufanya shughuli mbalimbali kuanzia tarehe 01 Disemba hadi 09 Disemba kwa kufanya usafi wamazingira katika eneo la soko la Mjimwema, kushiriki Michezo pamoja na kupanda miti katika eneo la Shule ya Chief Zulu Academy ambapo zoezi hilo liliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanal. Laban Thomas katika kilele cha maadhimisho hayo.
Kanal. Laban akizungumza na wananchi kwenye kongamano la kilele cha maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru Tanzania bara alisema” Mafanikio tunayoyaona yametokana na juhudi na nia ya dhati ya viongozi wetu walioongoza Taifa hili na wanaoendelea kuliongoza.”
Amesema “tunaposherehekea siku hii muhimu kwa namna ya pekee tumkumbuke kiongozi wa kwanza wa Taifa letu Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kazi kubwa aliyoifanya na kuwaongoza watanzania wakati wa kudai uhuru na kuhakikisha tunakuwa huru na kuunda Taifa hili wakati huo iliitwa Tanganyika.”
Amewataka wazazi na walezi wote kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2024 wahakikishe wanaripoti shule mara baada ya kufungua shule. “ Alisisitiza”
Kwa upande wa Manispaa ya Songea katika Sekta ya Elimu wakati wa Uhuru mwaka 1961 kulikuwa na Shule za Msingi sita zilizojengwa na Mkoloni ambazo ni Shule ya Msingi Matogoro – 1949, Shule ya Msingi Ruhila – 1929, Shule ya Msingi Tanga, Shule ya Msingi Lilambo, Shule ya Msingi Sinai na Shule ya Msingi Mlete.
Aidha, Baada ya Uhuru Maendeleo ya sekta ya elimu katika Manispaa ya songea tangu Tanzania ilipopata uhuru yamegawanyika katika Idara ya Msingi, Sekondari, vyuo vya kati na elimu ya juu, ambapo kwa upande wa Elimu Msingi Hata hivyo hadi kufikia mwaka 2023, halmashauri ya Manispaa ya Songea ina jumla ya shule za Msingi 101, ambapo shule 84 ni za Serikali na 17 ni za Taasisi binafsi (Private), sawa na ongezeko la 1583%.
Kwa upande wa Sekondari Wakati wa uhuru kulikuwa na shule ya sekondari 01 ambayo ilikuwa inamilikiwa na Serikali ambayo ni shule ya Wavulana ya Songea Boys iliyoanzishwa mwaka 1950 na serikali ya wakoloni kwa lengo la kuandaa viongozi watakao tawala pindi nchi itakapopata uhuru ambapo Mwaka 1961 shule hiyo ilikabidhiwa kwa Serikali ya Tanganyika.
Kuanzia miaka ya 2000 kutokana na Mpango wa Serikali wa kupanua Elimu kwa kujenga shule za kata ambapo shule zimeongezeka hadi kufikia, 2023 Manispaa ya Songea ina idadi ya shule za sekondari 43 zikiwemo za serikali 26 na zisizo za serikali 17.
Kwa upande wa sekta ya afya baada ya Uhuru Katika manispaa ya Songea, imeweza kufanikiwa ya kujenga Vituo vya kutolea huduma za afya, wigo wa upatikanaji wa huduma za afya, Watumishi wa kada za wataalamu wa afya na Huduma ya chanjo.
Miongoni mwa mafanikio katika Sekta ya Afya baada ya Uhuru ni pamoja na kuongezeka kwa Vituo 60 vya kutolea huduma za afya ngazi zote ikilinganishwa na kituo kimoja (1) mwaka 1960,
Kwa Upande wa huduma za miundombinu ya barabara Wilaya ya Songea baada ya Uhuru hadi sasa imefanikiwa kuwa na mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 2200.586 kati ya hizo, Kilomita 60.252 ni barabara za lami pamoja na taa za barabarani, kilomita 525.897 ni barabara za Changarawe, kilomita 1614.437 ni barabara za udongo na madaraja 150.
Hata hivyo baada ya uhuru hali ya barabara imeimarika kwa kiasi kikubwa ambapo kwa sasa mtandao wa barabara katika wilaya ya Songea imegawanyika katika makundi matatu ikiwemo na kilometa 1023.29 sawa na asilimia 46.5 za barabara zina hali nzuri, kilometa 307.91 sawa na asilimia 14 zina hali ya kuridhisha na kilomita 869.386 zina hali isiyoridhisha sawa na asilimia 39.5.
Kwa upande wa maji katika Manispaa ya Songea Mtandao wa bomba za usambazaji majisafi umeongezeka kutoka km 24 hadi km 568.511, Idadi ya wateja wa majisafi imefikia 22,343 ambao wote wamefungiwa dira za kupima maji, Mamlaka inayo matenki 11 yenye ujazo wa meta za ujazo 4,785 kati ya mahitaji ya meta za ujazo 20,593, pamoja na Uboreshaji wa mfumo wa ulipaji ankara za maji.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa