SHULE ya sekondari ya wasichana Songea(Songea Girls) imepewa na serikali shilingi milioni 220 za awamu ya kwanza kwa ajili ya kukarabati mabweni mawili.
Mkuu wa shule hiyo Tupoke Ngwala amewaambia wanahabari ambao wamefanya ziara ya kutembelea shule hiyo kuwa ukarabati huo unafanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambapo tayari wamekabidhi bweni moja la ghorofa ambalo limekarabatiwa kwa zaidi ya shilingi milioni 102.
Ngwala amesema bweni hilo ambalo linaitwa Mputa ni la ghorofa likiwa uwezo wa kuchukua wanafunzi 110 na kwamba hivi sasa kazi inayoendelea ni ya ukarabati wa bweni la pili linaloitwa Zulu.
“Ukarabati wa bweni lililomalizika ulianza Januari 10 mwaka huu na kwamba ukarabati wa bweni la pili umeanza tangu Aprili mwaka huu,lengo ni kukarabati mabweni yote matano kwa awamu’’,anasisitiza Ngwala.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa shule serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kufanyia ukarabati majengo yote ya shule hiyo yakiwemo mabweni na majengo ya utawala ili kuhakikisha shule hiyo inakuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia.
Hata hivyo amesema kabla ya serikali kutoa fedha hizo mabweni yalikuwa na hali mbaya ambapo kulikuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi ambao walikuwa wanalala katika vitanda vilivyochakaa ambapo serikali pia imetengeneza vitanda vipya 110 katika bweni ambalo limekamilika.
Shule ya sekondari ya wasichana Songea ni miongoni mwa shule kongwe nchini ina wanafunzi 874 wanaosoma kidato cha tano na sita ambayo ilianzishwa mwaka 1974.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 24,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa