SHULE ya sekondari ya wavulana Songea (Songea Boys) iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imewekwa katika mpango wa kuletewa kiasi cha shilingi milioni 325 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matano na mabweni matatu.
Timu ya wataalam wa Manispaa ya Songea ikiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo imetembelea shule ya sekondari ya wavulana Songea, eneo ambalo litajengwa madarasa matano na mabweni matatu.
Mhandisi wa Ujenzi katika Manispaa ya Songea Karoline Bernad amesema kati ya fedha hizo,shilingi milioni 100 zitatumika kujenga madarasa matano na matengenezo ya viti na meza 40 kila darasa ambapo jumla ya shilingi milioni 20 zinatarajia kutumika.
Kulingana na Mhandisi huyo,jumla ya shilingi milioni 225 zitatumika kujenga mabweni matatu yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 kila bweni na vitanda 40 (double decker) kwa kila bweni na kwamba kila bweni zitatumika shilingi milioni 75.
“Fedha hizi zitakavyoingia,zitapelekwa moja kwa moja shuleni,ujenzi huu utatumia force Account kwa mujibu wa maelekezo ya serikali,wahusika wakuu wakiwa ni Bodi ya shule’’,anasisitiza Bernad.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari katika Manispaa hiyo, Devota Luwungo,Bodi ya shule ya sekondari hiyo Juni 21 imepewa mafunzo elekezi na kusisitiza kuwa ujenzi wa madarasa hayo na mabweni unaanza mara moja mara baada ya fedha kuingia kwenye akaunti.
Amesisitiza kuwa hadi kufikia Agosti 30 mwaka huu,wanatarajia ujenzi wa madarasa na mabweni hayo utakuwa umefikia katika hatua za ukamilishaji na kwamba hivi sasa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano katika shule za sekondari za serikali zilizopo katika Manispaa ya Songea yanaendelea .
Anazitaja shule za sekondari za serikali za kidato cha tano zilizopo katika Manispaa ya Songea ambazo zinapokea wanafunzi kuwa ni Songea Girls,Songea Boys, Londoni, Msamala na Emanuel Nchimbi.
Serikali kupitia TAMISEMI imetenga shilingi bilioni 29 katika Halmashauri zote nchini ili kujenga miundombinu ya shule yakiwemo madarasa 478 na mabweni 269 ili kuhakikisha wanafunzi wote zaidi ya 20,000 waliokosa nafasi ya kupangiwa kidato cha tano,wanapata katika awamu ya pili.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 5,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa