Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
23 Desemba 2021.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefanya uzinduzi wa eneo la zaidi ya Hekari 200 lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda lililopo katika Kata ya Lilambo.
Tukio hilo limefanyika leo tarehe 23 Disemba 2021 lilioongozwa na Waziri wa Maliasili na utalii (Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini) Dkt. Damas Ndumbaro akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songea pamoja na viongozi kutoka Serikalini, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wataalamu kutoka Manispaa ya Songea pamoja na Wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo Ndumbaro amesema kuwa zoezi hilo limefanyika kufuatia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ilibeba dhana ya kuinua uchumi wa viwanda nchini Tanzania ambapo miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni uandaaji wa maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda ndani ya Manispaa ya Songea.
Dkt. Ndumbaro alisema kuwa kupitia mradi wa Benki ya dunia Manispaa ya Songea itaanza na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha uchakataji zao la Mahindi ambacho kitajengwa katika eneo hilo na kutoa fursa kwa wawekezaji wengine kuanza uwekezaji pamoja na kusaidia kutoa ajira kwa vijana na kuinua uchumi wa wananchi wa Manispaa ya Songea na Ruvuma kwa ujumla.
Aliongeza kuwa uwekezaji wa viwanda katika kata ya Lilambo unaenda sambamba na utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan lililotolewa kwenye kikao cha ALAT Taifa ambalo lilitaka asilimia 10% za mikopo ambazo zinatolewa na kila Halmashauri nchini kwa ajili ya kuwezesha vikundi mbalimbali, kuhakikisha zinatolewa kwa kulenga uwekezaji wenye tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa katika kutekeleza agizo hilo Halmashauri ya Manispaa ya Songea imeanza kwa kutenga maeneo rasmi ya uwekezaji wa viwanda pamoja na kutoa mkopo wa Tshs. Milioni 465 kwa vikundi 11, fedha ambazo zitasaidia kujenga kiwanda cha ushonaji, kiwanda cha utengenezaji wa batiki, kiwanda cha uchakataji maziwa, kiwanda cha Welding na Aluminium, kiwanda cha uchakataji wa mazao ya nyuki pamoja na jengo la Sanaa kwa ajili ya utalii.’ Dkt. Ndumbaro alibainisha’
Ametoa rai kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea kuviwezesha vikundi vyote vilivyopata mkopo huo kushiriki katika maonesho ya biashara kimkoa, kitaifa na kimataifa ili kuweza kupata fursa na uuzaji wa bidhaa zao pamoja na wawekezaji kutoka katika mataifa mbalimbali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kushika nafasi ya kwanza kati ya Halmashauri zote Mkoani Ruvuma kwa kuweza kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya wajasiriamali.
Amewataka wataalamu wa Manispaa ya Songea kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha vikundi ambavyo bado vinadaiwa mkopo kuhakikisha vinarejesha fedha hizo pamoja na kuwasisitiza wanakikundi waliopewa mkopo kuhakikisha wanarejesha fedha walizokopeshawa kwa wakati ili ziweze kusaidia kukopesha vikundi vingine ambavyo vinahitaji kupata mikopo hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Beno Philipo Mpwesa alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa Songea kupitia Idara ya Maendeleo ya jamii imefanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo na utoaji wa mikopo kwa asilimia 10% ambapo kwa mwaka 2021/2021 Milioni 314 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu ambapo kwa mwaka 2021/2022 Tshs milioni 465 zimetolewa kwa lengo la kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Alisema kuwa miongoni mwa changamoto zinazojitokeza katika utoaji wa mikopo hiyo ni pamoja na vikundi vingi vilivyochukua mikopo kushindwa kuendeleza miradi hali iliyopelekea kusambaratika kwa viundi hivyo na kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa China Africa Business Council Xian Qing ( kwa jina maarufu Komba), amempongea Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini kwa kuweza kuandaa eneo la uwekezaji wa viwanda ambapo ameahidi kutoa ushirikiano kwani ni miongoni mwa wawekezaji ambao watajenga viwanda vya kisasa katika eneo hilo pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wa Manispaa ya Songea ambapo katika kuunga mkono jitihada za Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt Damas Ndumbaro, mwekezaji huyo ametoa zawadi ya shilingi milioni tatu kwa wanamichezo wa Songea.
Miongoni mwa vikundi vilivyokabidhiwa hundi ya mikopo hiyo na Dkt. Damas Ndumbaro ni pamoja na kikundi cha Juhudi, Sayuni, Fahari, Jivunie, Tumaini, Mtazamo, Kazi iendelee, Wajasiriamali Investiment pamoja na Pambana Tutoke Group.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa