MILIONI 500 KUJENGA MRADI WA MAJI
ZAIDI ya sh.milioni 517 zinatarajia kutumika kujenga mradi wa maji wa Mitendewawa na kusambazwa katika mitaa miwili ya Mitendewawa na Chandarua iliyopo katika Kata ya Chandarua Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.Mhandisi wa Maji katika Manispaa ya Songea Eng.Samwel Sanya amemwambia Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema alipofanya ziara ya ukaguzi wa mradi huo kuwa utekelezaji wa mradi huo ulitakiwa kuanzia mwaka wa fedha wa 2014/2015,hata hivyo mradi ulichelewa kutokana na kuchelewa kwa fedha za mradi toka serikali kuu.
Eng.Sanya amesema utekelezaji wa mradi huo wenye urefu wa kilometa 13.4,ukiwa na vituo 13 vya maji, umeanza katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 ambapo Mkandarasi amefikia zaidi ya asilimia 60 ya utekelezaji.Amesema kisima cha mradi huo kina urefu meta 68 na kwamba uwezo wake ni kuzalisha maji ni lita 7000 kwa saa moja na kwamba wanufaika wa mradi huo ni wakazi zaidi ya 840.
Mkuu wa wilaya ya Songea mara baada ya kukagua mradi huo amemwagiza Mhandisi Sanya ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea kuhakikisha Mkandarasi anajenga mradi katika ubora na kumaliza kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika mapema.Mkoa wa Ruvuma unakadiriwa kuwa na wakazi 1,497,853 kati ya hao ni wakazi 851,034 sawa na asilimia 57 tu ndiyo wanaopata maji safi ni kwa mujibu wa takwimu za hadi Oktoba 2016.
Takwimu za mkoa wa Ruvuma zinaonesha kuwa,Katika maeneo ya vijijini wakazi wanaopata huduma ya maji safi ni asilimia 54.4,wakati wakazi wa mjini ni asilimia 68.1.
Taarifa imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa