Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
07.12.2021
Halmashauri ya Manispaa ya Songea yafikia asilimia 95% ya utekelezaji wa miradi ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano leo tarehe 07 Novemba 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Ruvuma pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Manispaa ya Songea kwa lengo la kujulisha umma juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea kutekelezwa pamoja na kutolea ufafanuzi juu ya mipango mkakati iliyopo katika kuboresha Manispaa ya Songea.
Mbano alianza kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa kiasi cha shilingi milioni 660,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 26 kwenye shule za sekondari na Msingi zilizopo ndani ya Manispaa ya Songea ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa maendeleo ya ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Aliongeza kwa kuwapongeza viongozi pamoja na wataalamu kwa kusimamia na kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati ndani ya mwezi mmoja na katika ubora unaotakiwa, ambapo hadi kufikia tarehe 10 Disemba 2021 Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea ataikabidhi miradi hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Songea, na ifikapo tarehe 15 Disemba 2021 miradi hiyo itakabidhiwa rasmi kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.’Alibainisha’
Alieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umesaidia katika kufungua uchumi wa wananchi hasa katika maeneo ambayo ujenzi unafanyika kwa kutoa ajira kwa vijana pamoja na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi ndani ya Manispaa ya Songea kuuza bidhaa zao kwa malipo ya uhakika.
Mbano aliendelea kubainisha kuwa pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Songea inaendelea na ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Lilambo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani yanayokusanywa pamoja na ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Msamala na kata ya Subira ambavyo vinajengwa kwa fedha kutoka Serikali kuu ambapo utekelezaji wa miradi hiyo ipo katika hatua ya msingi.
Aidha, alisema kuwa moja ya mpango mkakati uliopo ni kuboresha huduma za afya, elimu na miundo mbinu ndani ya Manispaa ya Songea ili kuhakikisha inatoka katika hadhi ya kuwa Manispaa na kufikia hadhi ya kuwa Jiji.’Mbano alisisitiza’
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dkt. Amosi Mwenda ametoa rai wananchi wa Manispaa ya Songea kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuendelea kupata chanjo ambayo inatolewa kwenye vituo vyote vya afya 33 vilivyopo ndani ya Manispaa ya Songea ambapo hadi sasa jumla ya watu elfu 19,700 ambayo ni sawa na asilimia 11.2% tayari wameshapata chanjo hiyo.
Akifafanua kuhusiana na mipango mbalimbali ya maendeleo ndani ya Manispaa ya Songea Afisa maendeleo ya jamii Martin Mtani amewataka wananchi kutumia fursa zilizopo hasa mikopo inayotolewa na Halmashauri ambapo kila mwaka shilingi milioni 350 zinatolewa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, fedha ambazo hurejeshwa bila riba.
Aliongeza kuwa kwa mwaka huu Halmashauri imejipanga kutoa mikopo yenye tija kwa wananchi ambapo jumla ya kiasi cha shilingi milioni 450 kitatolewa kwa vikundi mbalimbali kwa ajili ya utengenezaji wa viwanda vya ushonaji nguo, kiwanda cha uchakataji wa asali, kiwanda cha utengenezaji wa batiki pamoja na kiwanda cha mafundi welding ambayo itasaidia kuwainua wajasiriamali na kukuza uchumi wa Manispaa ya Songea.’Alibainisha’
Alisema Halmashauri ya Manispaa ya Songea itakuwa na utaratibu wa kuongea na Waandishi wa Habari kila baada ya miezi mitatu ili kuweza kutoa taarifa mbalimbali za Taasisi pamoja na kutangaza mafanikio yote ya Serikali yaliyotekelezwa na kutangaza miradi ya maendeleo.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa