IDARA ya Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na ofisi ya Maliasili na utalii Mkoa wa Ruvuma imeleta vipande viwili vya magogo yanayogeuka mawe kutoka pori la Selous na kuviweka katika Kituo cha Habari za Utalii cha Mkoa wa Ruvuma kilichopo ofisi za maliasili Mahenge mjini Songea.
Mara baada ya kufunguliwa rasmi Kituo cha Habari za Utalii cha Mkoa wa Ruvuma vipande vya magogo yanayogeuka mawe ni miongoni mwa vivutio adimu vya utalii ambavyo vimewekwa katika kituo hicho na kuvutia wengi wanaotembelea katika Kituo hicho.
Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Balthazar Nyamusya anatoa rai kwa watanzania kutembelea katika Kituo hicho na Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ili kujifunza rasilimali muhimu ya Taifa.
Miti inayogeuka mawe inatoka katika Pori la akiba la Selous lilianzishwa mwaka 1896 na wajerumani likiwa ni pori la kwanza kutengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori katika Bara la Afrika na la pili duniani kwa ukubwa baada ya hifadhi ya pori la Marekani ambalo linaitwa Yellowstone.
Mkurugenzi Mstaafu wa Uhifadhi ambaye pia amewahi kuwa Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori Kanda ya Likuyuseka katika Pori la Selous Ngwatura Ndunguru anaitaja Moja ya jamii ya miti ambayo haijafahamika na kutangazwa ipasavyo kuwa ni magogo ya miti iliyogeuka mawe ambayo kitaalam inaitwa fossilized tree trucks .
Kanda ya Kusini ya pori la Selous yaani Kalulu kwa mujibu wa Mhifadhi Kabanda Ismail ina umaarufu wa eneo lenye miti iliyogeuka kuwa mawe.Hali hiyo inatokana na hali ya kijiolojia inayotokea kwa mamilioni ya miaka na kuyageuza masalia ya miti kuwa mawe.
“Utafiti wa kiikolojia umebaini kuwepo kwa makaa ya mawe ambayo asili yake ni miti.Ukitembelea eneo hilo la mawe ya asili ya miti,utabaini picha halisi ya miti yaani matawi na maeneo ambayo matawi yake yalidondoka ambapo alama zake bado zipo hadi sasa hali ambayo inathibitisha ukweli wa kisayansi’’,anasisitiza Mhifadhi Ngwatura.
Utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa kivutio cha namna hii huwezi kukipata katika sehemu nyingine yeyote kusini mwa Jangwa la Sahara zaidi ya pori la Selous.
Hata hivyo utafiti wa kimataifa umebaini miti inayogeuka mawe iliyopo pori la Selous Tanzania inapatikana pia kaskazini mwa Afrika katika nchi za Misri,Libya na Algeria,pia miti hiyo inapatikana katika nchi ya Ugiriki na Marekani.
Makala imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa