NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
22.10.2021
Mkoa wa Ruvuma waandaa mkakati wa kuwapanga wajasiriamali wadogo (Machinga) katika maeneo rasmi ya kufanyia biashara.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge hapo jana tarehe 21 Oktoba 2021 alipokutana na viongozi mbalimbali wa Halmashauri zote 8, wadau na wafanyabiashara kutoka Mkoani Ruvuma katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Ibuge alibainisha kuwa mkakati wa kuwapanga wajasiriamali wadogo katika maeneo rasmi ni kufuatia utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye aliwataka wakuu wa Mikoa waratibu zoezi la upangaji wa machinga kwenye maeneo rasmi kwa lengo la kuepuka fujo, vurugu, migogoro pamoja na kudhibiti usafi endelevu wa mji husika.
Aliongeza kuwa viongozi wahakikishe maeneo watakayowatenga kwa ajili ya machinga kufanya biashara zao yanakuwa na miundombinu muhimu kama vyoo, maji na umeme pamoja na kuunda dawati maalumu la kuratibu shughuli za wamachinga kwenye Halmashauri husika ambapo amezitaka Taasisi zote kwenye Halmashauri husika kama TRA, TARURA,RUWASA, TANESCO, TANROADS na LATRA kushirikishwa kikamilifu ili kuweka miundombinu wezeshi ya upangaji wa Mji wa wamachinga katika maeneo rasmi ya biashara.
Alisisitiza kuwa zoezi la kuwapanga wamachinga katika maeneo rasmi ya kufanyia biashara liwe limekamilika ndani ya kipindi cha siku 90 kuanzia mwezi Novemba 2021 hadi tarehe 30 Januari 2022 ambapo amewataka viongozi kufanya kazi kwa uweledi na ifikapo Novemba 30 majadiliano ya uboreshaji kwa kuzingatia uwakilishi wa makundi yote yakiwemo viongozi wa wamachinga katika kuwashirikisha kwenye maeneo yao ili kuleta umoja.
Naye Mwenyekiti wa wamachinga Mkoa wa Ruvuma Salumu Sandali Masamaki ametoa shukrani kwa viongozi na Serikali kwa kuwapangia wamachinga maeneo rasmi ya kufanyia biashara ambapo alisema endapo mpango huo utakamilika wataweza kufanya biashara zao kwenye maeneo yenye utulivu na wapo tayari kutoa ushirikiano.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alieleza kuwa Manispaa ya Songea ina jumla ya wafanyabiashara 13,746 ambapo kati ya hao 2,746 wafanyabiashara wenye leseni na wanaolipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wafanyabiashara 11,000 ambao ni wafanyabiashara wadogo (Machinga) wanaofanya shughuli za biashara za Nafaka, Matunda, Mboga mboga, urembo, Nguo na viatu, Dagaa na vifaa vya umeme.
Alibainisha kuwa yapo maeneo ambayo wafanyabiashara wadogo wanafanya shughuli za biashara lakini hayajatengwa rasmi na Halmashauri kwa ajili ya Biashara ni pamoja na maeneo yote yanayozunguka soko kuu la Manispaa na wafanyabiashara wa barabara ya Litunu wanaozuia biashara za maduka, maeneo yote yanayozunguka soko la Manzese A na B, soko la kuku lililopo eneo la Mtini kwenye kiwanja cha Kanisa la Aglican, soko la viatu lilopo KAURU (kwenye geti la kituo cha Mafuta Kisumapai), Wafanyabiashara wadogo walioko ndani ya Stendi ya Mfaranyaki,soko la dagaa lililopo eneo la Versi (nyuma ya stendi ya Mfaranyaki), Wafanyabiashara wadogo nyuma ya kituo cha mafuta cha kisumapai pamoja na maeneo mengineyo.
Alisema kuwa Manispaa ya Songea imetenga masoko 3 kwa ajili ya kuwahamishia wafanyabiashara wakubwa wanaofanya biashara za jumla wa Mazao makavu, viazi na viazi, samaki na dagaa ambayo ni soko la mazao msamala, Mfaranyaki, Bombambili na Manzese A kwa lengo la kuwavutia wafanyabiashara wadogo katika masoko hayo, pia Halmashauri imepitia upya maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya wafanyabiashara na kutenga maeneo mapya pamoja na kuongeza masoko ya jioni kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.
Sagamiko alisisitiza kuwa maeneo yote waliyopangiwa wafanyabiashara wadogo katika Manispaa ya Songea kuna miundo mbinu muhimu kama choo, maji na umeme, hivyo basi ifikapo tarehe 30 Oktoba 2021 kila mfanyabiashara awe amehamia kwenye eneo lake na Ili kuhakikisha wafanyabiashara wadogo hawarejei kwenye maeneo yasiyo rasmi.
Alisema Kila Afisa Mtendaji kata, mtaa na Afisa afya wa Kata watasimamia maeneo hayo na kuhakikisha wafanyabiashara hao wanaendesha biashara zao katika maeneo waliyopangiwa na kuwa na takwimu sahihi za wafanyabiashara wadogo ifikapo tarehe 30/10/2021.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa