Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
23 MEI 2022
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt Frederick Sagamiko amefanya ziara ya kushtukiza na waandishi wa habari katika machinjio ya kisasa iliyopo ndani ya Manispaa ya Songea Kata ya Tanga.
Ziara hiyo ambayo ilifanyika Mei 21, 2022 kwa lengo la kukagua shughuli za uchinjaji wa nyama zinavyofanyika katika machinjio hiyo.
Akizungumza katika ziara hiyo Dkt Sagamiko alisema kuwa mfumo wa uchinjaji nyama katika machinjio hiyo ni wa kisasa ambao unatumia mtambo wa kuchinjia ambapo Manispaa ya Songea ni miongoni mwa miji michache nchini Tanzania ambayo inatumia mtambo huo..
Dkt. Sagamiko aliongeza kuwa kupitia machinjio ya kisasa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea yameongezeka na kuwataka wananchi kutumia nafasi zao mbalimbali kujenga Manispaa ya Songea kwa kuongelea vizuri miradi iliyotekelezwa na namna inavyofanya kazi kwa viwango na ubora unaotakiwa.
Alisema kuwa shughuli za uchinjaji nyama kwenye machinjio hiyo zinasimamiwa na kiongozi wa dini aliyeteuliwa na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kutoka Mkoa wa Ruvuma na hivyo nyama inayochinjwa katika machinjio hiyo ni halali na inafaa kutumiwa na wananchi wote.
Naye msimamizi wa Machinjio ya kisasa ya Manispaa ya Songea Said Renatus Sangije alisema kuwa machinjio hiyo ina uwezo wa kuchinja Ng’ombe 300 kwa siku ambapo kwa sasa inachinja Ng’ombe 35 hadi 40 tu kwa siku ambao bado hawakidhi mahitaji ya mtambo huo.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara wote ndani na nje ya nchi ya Tanzania kutumia fursa hiyo ya machinjio hiyo kwa kuendelea kupeleka Ng’ombe wengi zaidi kuchinja ili kwenda sawasawa na uwezo wa kuchinja wa machinjio hiyo.
Pia, Mchinjaji Mkuu wa Machinjio ya kisasa Shekhe alieleza kuwa uchinjaji nyama katika machinjio hiyo unazingatia taratibu zote za uchinjaji kwa kuzingatia misingi ya Imani ya Dini ya Kiislamu na kuandaliwa kwa ubora na usafi zaidi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tanga Agatoni Michael Goliama alisema kuwa machinjio ya Kisaa ya Manispaa ya Songea imeleta chachu ya maendeleo kwa wakazi wa kata ya Tanga kwa kutoa ajira kwa wananchi wake.
Nao wafanyabiashara wa nyama Manispaa ya Songea wametoa rai kwa wananchi kuendelea kutumia nyama inayochinjwa na machinjio hiyo kisasa kwa kuwa ni safi na salama kwa afya zao.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa