Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
16 JUNI 2022
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge amekabidhi hati miliki ya eneo la jumla ya hekari 65 lililopo Kata ya Tanga Mtaa wa Pambazuko Manispaa ya Songea kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu cha Uhasibu Arusha-Tawi la Songea hapo jana Juni 15, 2022.
Akizungumza wakati akimkabidhi hati miliki hiyo, Brig. Jen Ibuge “ameishukuru Serikali ya Awamu ya 6 kwa kuhakikisha inatoa fursa ya kuwezesha wananchi kunufaika katika nyanja tofauti ambapo kupitia Wizara ya Elimu zitatolewa fedha ambazo zitasaidia kukamilisha ujenzi wa chuo hicho Mkoani Ruvuma ambacho kitakuwa na uwezo wa kuwa na wanafunzi zaidi ya elfu nne (4000)”.
Ametoa wito kwa Mkuu wa chuo hicho kuhakikisha wanaanza hatua za awali za ujenzi kwa kuwa baadhi ya changamoto zilizokuwa zinakabili eneo hilo ikiwemo na ukosefu wa umeme na maji tayari zimeshatatuliwa na mamlaka husika.
Ibuge ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kushikamana kwa kuhakikisha wanashiriki katika maendeleo chanya ya Mkoa wa Ruvuma ambapo kupitia ujenzi wa chuo hicho utafungua fursa ya ajira pamoja na kuongeza kipato kwa biashara.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha Dkt. Mwaitete Cairo ametoa shukurani kwa uongozi wa Mkoa wa Ruvuma ambapo alisema kuwa ujenzi wa chuo hicho utasaidia kupunguza uhitaji wa elimu ya juu kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuunga mkono jitihada za Serikali pamoja na sera ya nchi inayozingatia utoaji wa elimu bora kwa wananchi.
Aliongeza kuwa ujenzi wa chuo hizho unatarajia kuanza rasmi mwezi Julai 2022 ambapo hadi sasa hatua za awali za ujenzi zimeanza ikiwemo na uandaaji wa michoro ya ujenzi huo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa bodi ya chuo cha Uhasibu Arusha CPA Joseph Mwiguru alisema kuwa chuo kimejipanga kutoa elimu bora kwa wanafunzi watakaodahiliwa katika chuo hicho wa ndani ya Mkoa pamoja na nchi jirani na Mkoa wa Ruvuma.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Hamisi Abdallah Ally ameahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi wa chuo hicho ili kufanikisha ujenzi wa chuo kwa haraka ikiwa ni utekelezaji wa sera ya elimu kupitia Ilani ya CCM ambayo inatoa kipaumbele kwa utoaji elimu kwa wananchi wake.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt Frederick Sagamiko alisema Manispaa ya Songea imekamilisha hatua ya upimaji wa eneo pamoja na uandaaji wa hati miliki.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa