Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewataka Wataalamu kufanya kazi kwa weredi na kutekeleza vizuri jukumu la kukusanya kazi data za walipa kodi za majengo, mabango na kugawa vitambulisho vya wajasiliamali wadogo.
Christina ametoa agizo hilo jana 12 machi 2021 kwenye kikao kilichohudhuriwa na Wakurugenzi wa Halmashauri zote Mkoani Ruvuma, Maafisa biashara, Maafisa Tehama, pamoja na makatibu tawala kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kwa lengo la kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kufanikisha kwa zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wajasiliamali wadogo kwa kutumia mfumo wa ulioandaliwa na ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na mamlaka ya Mapato Tanzania TRA.
Alisema awali kodi za majengo zilikuwa zikikusanywa na Serikali za mitaa, kuanzia julai mosi 2017 jukumu hilo walipewa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kwa sheria ya fedha namaba 4 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017. kupitia kikao kazi cha tarehe 05 februari 2021 ofisi ya Rais TAMISEMI ilirejesha ukusanyaji wa kodi za majengo, ugawaji wa vitambulisho vya wajasiliamali wadogo na ushuru wa mabango kutoka kwa mamlaka ya mapato Tanzania kwenda kwa Serikali za mitaa.
Alibainisha kuwa mwaka 2020 Mkoa wa Ruvuma ulipokea vitambulisho 58,000 na kufanikisha kugawa vitambulisho 23256 kwa kutumia mfumo wa ugawaji wa vitambulisho ulioandaliwa na ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo kati ya hivyo vitambulisho 34744 vimebaki.
Akitoa pongezi kwa Halmashauri ya Mbinga ambayo imefanikiwa kugawa vitambulisho 4768 kati ya vitambulisho 6500 sawa na asilimia 53% huku Halmshauri nyingine zikiwa chini ya wastani 50%. Ameagiza Halmashauri zote Mkoani Ruvuma kurudisha haraka vitambaulisho vilivyobakia vya kipindi cha mwaka 2020 ili viweze kurudishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Alisema mwaka 2021 Mkoa wa Ruvuma umepewa vitambulisho 56,000 ambapo tayari mgawanyo wa vitambulisho hivyo umeshafanyika ambapo Manispaa ya Songea imepewa vitambulisho 10600, Tunduru vitambulisho 10200, Namtumbo vitambulisho 7700, Mbinga mji vitambulisho 6300, Mbinga 6300, Nyasa vitambulisho 7700, Madaba vitambulisho 3900 na halmashauri ya Wilaya ya Songea vitambulisho 3300.
Amewataka Wataalamu hao kusimamia vizuri ukusanyaji wa kodi za majengo ikiwemo na utunzaji wa takwimu za mabango sambamba na utoaji wa elimu kwa walipa kodi ili kuwajengea uelewa wananchi wa ulipaji wa kodi zamajengo, na mabango.
Mwisho alitoa wito kwa wajasiliamali yeyote atakayekuwa amepewa kitambulisho kutobugudhiwa au kunyanyaswa na mtu yeyote kwani atakuwa ametambulika rasmi kupitia kitambulisho alichokuwa nacho. Alisisitiza.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
13.03.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa