Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Dr. John Pombe Magufuli imejidhatiti katika kuboresha huduma za afya nchini, ikiwemo na kutoa huduma za upimaji wa VVU, huduma ya Tohara kwa wanaume, pamoja na kuimarisha kamati za UKIMWI za kata na mitaa ili kutokomeza au kupunguza maambukizi mapya ya Virus vya Ukimwi.
Hayo yametamkwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet kamando Mgema kwaniaba ya Dr. Damas Ndumbaro (Mbunge Jimbo la Songea Mjini) katika maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 01 disemba Duniani kote, ambayo kiwilaya maadhimisho hayo yamefanyika katika kata ya Mshangano Manispaa ya Songea.
Awali mgeni rasmi alianza kukagua vibanda vya maonesho mbalimbali vya wadau wa mapambano dhidi ya Ukimwi ikiwemo na dawati la jinsia na watoto (Ruvuma), Inter Care Organization (ICO), ICHF under five 5, PAD pamoja na banda la upimaji wa virus vya ukimwi (VVU).
Pololet aliwapongeza wale wote waliothubutu kwenda kupima VVU na kujua hali ya afya zao ambapo katika maadhimisho hayo watu 128 walijitokeza kupima VVU, wanaume 79 na wanawake 49 kati ya hao hakuna aliyekutwa na maambukizi ya VVU.
Alisema lengo kuu la Serikali ni kutoa elimu dhidi ya maambukizi ya VVU na namna ya kujikinga na kuwakinga wengine ili maambukizi yasiweze kuenea Zaidi, pamoja na kutoa elimu ya namna ya kuzuia kuenea kwa VVU katika jamii.
Amewaasa wale wote wenye maabukizo ya Virus Vya Ukimwi kufuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo kuanza dawa mara moja na kwa usahihi bila kuacha.
Akizitaja faida za kupima na kutambua afya zao ambapo alisema, itawasaidia kujiunga na kupata dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV), atakuwa amepata maelekezo ya matumizi sahihi ya dawa za ARV hususani ( wamama wajawazito), pamoja na kufahamu namna ya kuzuia maambukizi kwenda kwa wengine. ( Pololet alibainisha).
Naye Mratibu wa kudhibiti UKIMWI (TIBA) Manispaa ya Songea Felista Kibena alisema “ katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2020 jumla ya watu 57232 walipimwa afya zao, hivyo wanaume 33037 na wanawake 24195 kati ya hao wanaume 905 na wanawake 1344 walikutwa na maambukizo ya VVU sawa na asilimia 3.9% na hao wote wamefanikiwa kuunganishwa kwenye huduma ya tiba na matunzo katika vituo vya CTC.”
Kibena aliongeza kuwa katika kipindi cha 2019 hadi 2020 jumla ya akina mama 8572 wamepimwa afya zao na kati ya hao kina mama 166 waligundulika na VVU sawa na asilimia 1.9 %, na wote wameanza dawa za kufubaza makali ya VVU ( ARV).
Aidha, Manispaa ya Songea inaendelea kutoa Elimu kwa jamii juu ya kujikinga na maambukizo ya virus vya ukimwi pamoja na kutoa elimu sahihi ya matumizi ya sahihi ya kondomu na kuzisambaza kwa watumiaji kwa kutumia watoa huduma na waelimishaji rika kwa kata zote 21 na mitaa 95.
Kauli mbiu” MSHIKAMANO WA KIMATAIFA, TUWAJIBIKE KWA PAMOJA.”
IMETAYARISHWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABRI MANISPAA YA SONGEA.
01.12.2020
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa