Na;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI
MANISPAA YA SONGEA.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema, amewataka Wananchi wa Manispaa ya Songea kufuata sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004 ambayo inasisitiza kuwa kutoka kwenye kingo za Mito kwa pande zote mbili hadi mita 60 ni vyanzo vya maji.
Kauli hiyo imeelezwa leo tarehe 06.04.2022 wakati akizungumza na Wananchi wa Manispaa ya Songea akiwa katika hatua ya utekelezaji wa zoezi la upandaji wa miti katika Bonde la Mto Ruhila lililopo kata ya Seedfarm kwa lengo la kutunza chanzo cha Maji Ruhila ( SOWASA) lililoshirikisha wanafunzi, Waheshimiwa Madiwani, Wataalamu na wananchi.
Pololet alisema “ awali maeneo hayo yalikuwa ni sehemu ya shughuli za kibinadamu pamoja na makazi ya watu, baadae Serikali ilitoa shilingi Bilioni 1.9 kulipa fidia kwa wananchi wa eneo la Mabonde kama Mahilo, Chemchem, pamoja na Ruhila ili kutunza uoto wa asili wa mazingira ya chanzo cha Maji Ruhila.”
Aliongeza kuwa baada ya kuwaondoa wananchi hao, amezitaka Mamlaka husika kama SOWASA, TFS, pamoja na Idara ya Maliasili kutekeleza wajibu wao kwa kuweka ulinzi imara wa maeneo kwa kuweka mipaka inayoonekana, pia alama hizo zitumike kama katazo la mtu yeyote kuzivuka na kwenda kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya eneo linalohifadhiwa.
Amewarai wananchi wa Manispaa ya Songea hususani waishio jirani na Bonde la la Mto Ruhila ikiwemo na shule ya Wavulana ya Songea ambayo ipo jirani na bonde hilo kuhakikisha wanaimarisha ulinzi katika kunza chanzo hicho kwa manufaa ya jamii yote ya Songea.
Amempongeza Waziri wa Sheria na Katiba ambaye pia ni Mh. Mbunge wa jimbo la Songea Mjini pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Mary Massanja kwa kuwatia moyo wananfunzi wa shule ya Sekondari ya Wavulana Songea kwa kuanzisha vikundi vya utunzaji wa vitalu vya miti ambapo vikundi hivyo vimeweza kuatika miche ya miti elfu hamsini 50,000 ambayo imetumika kupandwa katika bonde la mto Ruhila. Pololet “ alipongeza”
Amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea kushirikiana na Taasis mbalimbali kama TFS, na Idara ya Maliasili ambayo ipo chini ya Halmashauri, kuhakikisha wanaotesha miche ya miti na kuweka Mpango thabiti kwa kila mkuu wa Idara aweze kupewa kata kwa kushirikisha waheshimiwa Madiwani wa kata husika kuhakikisha upandaji wa miti unafanyika samabamba na kutunza miti hiyo. Alisisitiza.
Naye Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano, amewataka wananchi wote wa Manispaa ya Songea kuhakikisha wanapanda miti aina ya miparachichi ambayo itasaidia kuinua kipato cha familia.
Afisa Misitu Manispaa ya Songea Godfrey Luhimbo, amesema miti iliyopandwa katika chanzo cha Maji Ruhila itasaidia kuweka mazingira mazuri ambayo yataweza kuimarisha uoto wa asili, ikiwa katika zoezi hilo miti aina ya Minyonyo 3000 imepandwa.
Nao wanafunzi wa Shule ya Wavulana Songea kwa umoja wao wamesema wataitunza miti hiyo kwa kuhakikisha isiweze kuungua moto kwa manufaa ya jamii ijayo.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa