Wilaya ya Songea ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Kapenjama Ndile wamefanya kikao cha kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Songea ambacho kimefanyika tarehe 19 Januari 2024 kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali Wilayani humo pamoja na kupokea ushauri na changamoto zilizojitokeza ngazi ya Wilaya ya Songea.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali ngazi ya Wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Songea, Wenyeviti wa Halmashauri ya Madaba, Songea, Manispaa ya Songea, Wakuu wa Idara, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini pamoja na wadau mbalimbali kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Wilman Kapenjama Ndile amesema, Serikali imetengeneza utaratibu na miundo mbalimbali wa kukutana na kukusanya mawazo na ushauri kutoka kwa wadau hususani kwa Wilaya husika ambapo huwezesha kutatua changamoto na kuleta maendeleo kwa jamii.
Alisema Serikali imejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Songea kwa kuhakikisha wanapeleka huduma muhimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali hasa miundombinu ya umeme, maji, elimu na afya, mazingira na kilimo hususani zao la Miwa. “Alibainisha.”
Aliongeza kuwa kupitia kiwanda cha miwa kinachotarajia kujengwa katika kijiji cha Magwamila katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea kitawezesha kuniua pato la Taifa, Kuimarika kwa miundombinu ya barabara pamoja na fursa za ajira kwa Wananchi.
Aidha amewataka wataalamu kuandaa kikao kingine ambacho kitalenga kuandaa wasilisho la Sekta ya madini ngazi ya Wilaya ambayo itasaidia kufahamu kupata takwimu ya misitu iliyopo, ikiwemo na sekta ya ardhi katika zoezi la upimaji wa ardhi ambao utawezesha kufahamu idadi ya viwanja kulingana na ongezeko la jamii inayohitaji viwanja.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini Mwinyi Msolomi amewataka wataalamu kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa maendeleo wa mwaka mmoja ambao utawasilishwa katika kikao na kujadiliwa ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali za jamii kupitia Halmashauri husika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakurugenzi wa Halmashauri zote 3 zilizopo ndani ya Wilaya ya Songea, ambapo wameahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zao.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa