Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
13 JUNI 2022
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema ameongoza kikao kazi cha kamati ya Sensa ya Wilaya ya Songea leo tarehe 13 Juni 2022 kwa lengo la kupokea taarifa ya maandalizi ya sensa ya watu na makazi katika Wilaya ya Songea.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, viongozi wa mila pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Akizungumza katika kikao hicho, Mgema ameitaka kamati hiyo inaleta ushirikiano katika kuhakikisha wanasimamia zoezi la uhamasishaji kwa wananchi kwa kutoa elimu kupitia mikutano mbalimbali, nyumba za ibada, mikusanyiko mbalimbali, na vyombo vya Habari kuhusiana na zoezi la SENSA ya watu na makazi ambalo linatarajiwa kufanyika ifikapo Agosti 23 mwaka huu.
Mgema alisema kuwa kila mwananchi anatakiwa kutambua na kushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa sahihi ikiwemo na idadi ya watu katika kaya husika kwa mujibu wa sheria ya Takwimu kwa lengo la kufanikisha na kuchochea kasi ya maendeleo ya watu na makazi yao. “Mgema Alisisitiza”
Akiwasilisha taarifa ya maandalizi ya sensa ya watu na makazi Manispaa ya Songea, Mratibu wa sensa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Upendo Bonomali alisema kuwa Manispaaya Songea imetenga maeneo 477 ya kuhesabia watu pamoja na kuunda kamati za sensa ngazi ya kata zote 21 na mitaa 95.
Aliongeza kuwa Manispaa ya Songea imefanya uhamasishaji wa zoezi hilo kwa jamii kupitia matamasha mbalimbali, kugawa vipeperushi vinavyotoa elimu ya sensa kwa jamii, kutoa elimu kwa Madiwani, watendaji wa kata, wenyeviti wa mitaa na mabalozi kupitia vikao mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kupitia vikao vya kisheria katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mratibu wa Sensa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Prosper Romanus Luambano alisema kuwa hadi sasa wameandaa maeneo 170 ya kuhesabia, kuhamasisha jamii kupitia vikao mbalimbali vya kisheria, kugawa vipeperushi pamoja na kuunda kamati za sensa kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji na kata.
Pia, Mratibu wa Sensa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Zainabu Mbaruku Hamidu alibainisha kuwa zoezi la uhamasishaji jamii linaendelea kufanyika kupitia matamasha ya michezo, vikao mbalimbali, mikutano , ugawaji wa vipeperushi pamoja na uundaji wa kamati za sensa kwa ngazi zote.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano alisema kuwa kamati za kata zinatakiwa kuweka wawakilishi ambao ni viongozi wa dini ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi la uhamasishaji kwa jamii.
Naye Katibu wa Baraza la Waislamu Mkoa wa Ruvuma (BAKWATA) Shekhe Rajabu Songambele ametoa shukrani kwa uongozi ngazi ya Wilaya kwa kuandaa kikao cha uandaaji wa kamati ya uhamasishaji wa SENSA ya watu na makazi pia ameahidi kutoa ushirikiano katika kutekeleza na zoezi hilo.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa