MRADI wa Ujenzi wa machinjio ya kisasa unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma ambao umefikia zaidi ya asilimia 75 ukikamilika unatarajia kuongeza ajira kwa wananchi wa Manispaa ya Songea. Mradi huo ambao unagharimu zaidi ya sh.bilioni 3 unatarajia kukamilika Julai mwaka huu.
Akitoa taarifa ya mradi Kaimu Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa ya Songea Mhandisi Nicolus Danda amesema mradi wa machinjio ya kisasa unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni tatu.
Amemtaja Mkandarasi wa mradi huo ambaye hadi sasa amelipwa shilingi milioni 400 kuwa ni Kampuni ya Giraffe ambapo mkataba wake ni wa mwaka mmoja ambao umeanzia Julai 2017 na kukamilika Juni 30, 2018.
Kwa mujibu wa Danda kazi ambazo zinafanyika kwenye mradi huo ni ujenzi wa machinjio yenye urefu wa meta 64 na upana wa meta 24,ujenzi wa zizi lenye uwezo wa kuhifadhia ng’ombe 200 na ujenzi wa uzio,tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita ya 162,000.
Kazi nyingine anazitaja kuwa ujenzi wa nyumba mbili ikiwemo ya daktari wa mifugo na mlinzi,ujenzi wa barabara ya kilometa moja ambayo itazunguka eneo la mradi na ujenzi wa maeneo ya kupaki magari. Mkandarasi huyo ameahidi kumaliza kazi ndani ya mkataba ambapo amesema hivi sasa imebakia mistari michache kukamilisha kuzungusha jengo hilo.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni Mosi 2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa