Na;
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
18 MEI 2022
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Mhe. Michael Mbano amewataka wenyeviti wote wa Serikali za mitaa Manispaa ya Songea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika ifikapo Agosti 23 mwaka huu.
Ameyasema hayo katika kikao kazi na wenyeviti wa mitaa 95 ya Manispaa ya Songea hapo jana tarehe 17 Agosti 2022 kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kwa lengo la kujadili namna ya kuboresha wa utendaji kazi katika ngazi ya mitaa kwa kufuata kanuni na taratibu za utawala bora.
Mbano alisema kuwa kufanyika kwa sensa ya watu na makazi mwaka huu kutasaidia kupata takwimu sahihi za idadi ya watu ndani ya Manispaa ya Songea hali ambayo itarahisisha zoezi la ugawaji wa kata na mitaa kwa maendeleo ya wananchi kwa ujumla.
Aliongeza kuwa kila mwenyekiti wa Serikali za mitaa atumie fursa ya vikao vinavyofanyika katika maeneo yao kuhamasisha wananchi kutoa taarifa zao sahihi ili kuiwezesha Serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, elimu pamoja na miundombinu ya barabara.
Pia amewataka wenyeviti hao kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu inayoendelea kuwekwa kwa ajili ya utambulisho wa anuani za makazi ikiwemo na nguzo za barabara za mitaa katika maeneo yao pamoja na kuhakikisha kila mwananchi anaweka kibao cha anuani za makazi katika nyumba yake ambapo amewataka wenyeviti kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa zoezi hilo.
Mbano ametoa rai kwa wenyeviti hao kusimamia ulinzi na usalama wa wananchi pamoja na mali zao kupitai kamati za ulinzi na usalama kwenye mitaa kwa lengo la kudhibiti wimbi la matukio ya wizi ndani ya Manispaa ya Songea.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Christopher Ngonyani alisema kuwa kuanzia mwezi julai mwaka huu Manispaa ya Songea imejipanga kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuwataka wenyeviti wa mitaa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ndani.
Amewataka wenyeviti hao kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa (ICHF iliyoboreshwa) ili kuwasaidia wananchi kupata huduma bora za afya kwa gharama nafuu.
Ngonyani ametoa wito kwa wenyeviti wa Serikali za mitaa kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kuwezesha kujenga ofisi ya Serikali za mitaa bila kusubiri kujengewa na Halmashauri, kwa kufanya hivyo kutasaidia Halmashauri kuendelea vyema katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.”Alisisitiza”
Amewaelekeza viongozi hao kutumia fursa za utekelezaji wa miradi ya Tasaf inayotarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kuhamasisha wananchi wote kushiriki katika zoezi la kuibua miradi ambayo itatekelezwa na kaya lengwa ili kupunguza umaskini pamoja na kuleta maendeleo katika mitaa yao.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Abdul Mohammed Mkalipa amewataka wenyeviti wa Serikali za mitaa kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya 6 kwa kutoa ushirikiano ili kuleta maendeleo kwa wananchi pamoja na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Naye Mwenyekiti wa wenyeviti wote wa Manispaa ya Songea Issa Hamza Zawamba ametoa rai kwa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuboresha utoaji wa stahiki za wenyeviti hao pamoja na kupewa vitambulisho maalumu kwa lengo la kuboresha mazingira yao ya utendaji kazi.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa