Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Isabela Chilumba amekagua Msitu wa Hifadhi ya asili ya Chiwindi yenye ukubwa wa hekta 3000 iliyopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji na kubaini uchafuzi unaofanywa na shughuli za kibinadamu.
Uchunguzi umebaini kuwa kuna uchafuzi wa kutisha ndani yake hifadhi hiyo ambapo mto Chiwindi uliopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji,unaopita ndani ya hifadhi hiyo umechafuliwa katika kiwango cha kutisha.
Mto huo ambao unamwaga maji yake ziwa Nyasa ni mchafu kwa mwaka mzima kutokana na kuchafuliwa na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu toka nchi zote mbili ambao wanatumia kemikali ya zebaki kusafishia dhahabu.
Taarifa ya Ofisi ndogo ya Bonde la Maji la ziwa Nyasa inaonesha kuwa kati ya mito mikubwa minane inayoingiza maji katika ziwa Nyasa,mto Chiwindi unaoongoza kwa uchafuzi wa taka zenye sumu ambazo zinaleta athari kubwa kwa binadamu na viumbehai wa mtoni na ziwa Nyasa.
Utafiti umebaini ziwa Nyasa linapokea takataka mbalimbali ikiwemo taka zenye sumu kutoka katika mito inayomwaga maji katika ziwa hilo na kusababisha kina cha maji kupungua.
Mito mitano inayoongoza kwa kusomba mchanga na tope na kutumbukiza ndani ya Ziwa Nyasa ni mto Ruhuhu wenye ukubwa wa mita za mraba13,490,mto Songwe mita 3,550, mto Rufirio mita1,350, mto Kiwira mita 1,660 mto Lumbira mita 1,414 na mto Chiwindi.
Mto Ruhuhu ambao chanzo chake ni Mkoa wa Njombe na Ruvuma umechafuliwa na maji yake yanaonekana kuwa na tope kwa mwaka mzima kutokana na shughuli za kilimo na uchimbaji wa madini ambao unafanywa na wakazi ambao wanaishi kando kando mwa mito hiyo.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa