Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
13.04.2022
Kiongozi wa mbio maalumu za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Sahili Nyanzabara Geraruma amezindua na kukagua jumla ya miradi 9 yenye thamani ya Shilingi Billion 1,218,600,000 ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea ikiwa ni fedha kutoka Serikali kuu, tozo na mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na nguvu za wananchi.
Akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi wa shughuli za ujenzi unaoendelea wa viwanda vidogo vya wajasiriamali kata ya Lilambo, kiongozi huyo ametoa wito kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuendelea kujitokeza na kuomba mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi wao binafsi pamoja na Taifa kwa ujumla.
Geramura ameipongeza Halmashauri ya Manispaa Songea kwa kuhakikisha watu wa makundi maalumu wanaendelea kunufaika na asilimia 10% ya fedha kutoka mapato ya ndani kwa kutoa mikopo bila riba pamoja na kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa viwanda ambavyo vitatoa fursa za ajira kwa wanakikundi na wananchi kwa ujumla.
Amewataka viongozi kuendelea kusimamia na kuhakikisha ujenzi wa viwanda hivyo unazingatia ubora unaotakiwa ambapo hadi sasa majengo 5 tayari yamekamilika ikiwemo na kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki, kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, kiwanda cha kutengeneza batiki, kiwanda cha ushonaji nguo pamoja na kiwanda cha kuchomelea vyuma na Aluminium.”Alisisitiza”
Aidha, miradi mingine iliyotembelewa na Mbio maalumu za Mwenge wa Uhuru ni pamoja na uzinduzi wa madarasa 2 shule ya Sekondari Lizaboni, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara katika eneo la bohari ya Serikali, kuweka jiwe la msingi Kituo cha Afya Msamala pamoja na ukaguzi wa mabanda ya rushwa, dawa za kulevya na elimu ya sensa, ambapo miradi yote imeridhiwa na kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 inasema “SENSA NI MSINGI WA MIPANGO YA MAENDELEO, SHIRIKI KUHESABIWA TUYAFIKIE MAENDELEO YA TAIFA”
Mwenge wa Uhuru Manispaa ya Songea umepokelewa tarehe 12 Aprili 2022 katika kijiji cha Likuyufusi na kukabidhiwa Halmashauri ya Wilaya Madaba 13 Aprili 2022.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa