Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
06.10.2021
Naibu Waziri ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Mheshimiwa Deogratius Ndejembi (MB) amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanafanya kazi kwa ueledi.
Ndejembi ameyasema hayo alipofanya ziara katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea na kuzungumza na watumishi wa umma kutoka Idara mbalimbali ndani ya Manispaa ya Songea leo tarehe 06 Oktoba 2021 kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao katika utendaji wao wa kazi.
Akijibu changamoto zilizotolewa na watumishi hao, Ndejembi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya sita imeweka kipaumbele katika kuhakikisha watumishi wote wa umma wanapata maslahi yao ili kuchochea utendaji kazi katika kuleta maendeleo kwa wananchi ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja upandishaji wa madaraja na mishahara, kutoa ajira kwa walimu hasa walimu wasayansi katika shule za msingi na sekondari, madai ya mishahara pamoja na malipo ya wastaafu kwa kufuata madaraja yao husika.
Ndembeji amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanapodai stahiki na haki zao kwa Serikali na wao wawe wametimiza wajibu wao kama watumishi kwa wananchi wanaowatumikia katika maeneo yao ya kazi kwa kufanya kazi kwa bidii na katika misingi ya nikidhamu na uadilifu.”Alisisitiza”
Ameongeza kuwa ushirikiano kwa watumishi wa umma ni jambo la kuzingatiwa ili kuleta maendeleo yenye tija katika Halmashauri husika lakini pia kwa wananchi wake na kuwataka watumishi wote kuacha majungu na maneno yasiyofaa mahala pa kazi na badala yake kuongeza juhudi katika utendaji wa kazi kwa umoja.
Ndembeji amezitaka Halmashauri zote kuhakikisha zinatatua changamoto mbalimbali za wananchi kama vile migogoro ya ardhi pamoja na kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Pia amemtaka Afisa utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakikish anafanya uhakiki wa madeni yote ya Watumishi na hadi kufikia tarehe 22 Oktoba 2021 awe amewasilisha majina ya watumishi wote wenye madai katika ofisi ya Raisi utumishi.”Alisisitiza”
Ametoa rai kwa watumishi wote wa umma kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO 19 ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo ili kuwa mfano bora kwa jamii inayowazunguka na kuweza kuwahamsisha wananchi kupata chanjo hiyo.
Kwa upande wake Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano amemshukuru Naibu Waziri huyo kwa kutembelea Halmashauri ya Manispaa ya Songea pamoja na kuhaidi kuyafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa