Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
17.12.2021
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mh. David Ernest Silinde amefanya ziara ya siku moja ndani ya Manispaa ya Songea kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19.
Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 17 Disemba 2021 ambapo katika ziara hiyo, aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, wataalamu pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Manispaa ya Songea.
Silinde alisema kuwa lengo la kufanya ziara hiyo ni kufanya ukaguzi wa miradi ili kujiridhisha na kuhakiki fedha zilizotolewa na Serikali kiasi cha shilingi milioni 660 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 29 kwa shule za sekondari na vituo shikizi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea kama zimefanya kazi kama ilivyokusudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.’Alibainisha’
Aliongeza kuwa bilioni 304 zilitolewa kwenye Halmashauri mbalimbali nchi nzima kwa lengo la kujenga miundombinu ya elimu ambazo zimeweza kujenga vyumba vya madarasa elfu kumi na tano (15000) tayari vimejengwa, madarasa ambayo yatasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari na vituo shikizi.
Ametoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko , wakuu wa shule na kamati za ujenzi kwa usimamizi mzuri wa miradi ambayo ni mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 ambao umekamilika tayari kwa matumizi kwa asilimia 100% katika ubora uliotakiwa kama ilivyoagizwa na Serikali.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alisema kuwa miongoni mwa mikakati iliyosaidia kukamilisha utekelezaji wa miradi ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 kwa asilimia 100% ni pamoja na kufanyika kwa mikutano ya utambulisho wa miradi kwa wananchi, kukutana na wakuu wa shule na kamati za ujenzi kwa lengo la kujadili namna ya kutekeleza mradi kwa wakati, kukutana na wafanyabiashara wauzaji wa vifaa vya ujenzi waliopo Manispaa ya Songea kwa ajili ya kurahisisha ununuzi wa vifaa vitakavyotumika katika utekelezaji wa mradi pamoja na kuunda timu ya ufuatiliaji ngazi ya Halmashauri na kata.’Alibainisha’
Dkt. Sagamiko ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Songea kwa kutoa maelekezo thabiti juu ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Afisa elimu Mkoa wa Ruvuma Juma Fuluge alieleza kuwa Mkoa wa Ruvuma ulipokea zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 448 katika shule za sekondari, vyumba vya madarasa 52 kwenye vituo shikizi pamoja na mabweni matatu 3 katika shule za sekondari.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma una jumla ya shule za sekondari 214 pamoja na shule za msingi 818 ambapo mradi huu wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 umesaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika shuleza sekondari Mkoani Ruvuma kwa Zaidi ya asilimia 80%.
Amewarai wakuu wa shule kuhakikisha wanasimamia na kutunza miundombinu ya madarasa yaliyojengwa pamoja na samani zake ili kuhakikisha inatumika kwa manufaa ya watoto watakaondelea na masomo katika shule hizo.
Ametoa wito kwa wananchi Mkoani Ruvuma kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa kupata chanjo ya ugonjwa huo kwa hiyari.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa