Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
29 JULAI 2022
Naibu Waziri Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Pinda ameongoza kikao cha Kamati ya watoa huduma ya msaada wa kisheria Mkoani Ruvuma leo tarehe 29 Julai 2022.
Akizungumza katika kikao hicho, Pinda alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa sheria ya utoaji huduma ya msaada wa kisheria ni kuhakikisha inasaidia wananchi wanapata haki ya huduma ya kisheria bure pamoja na elimu ya sheria kwa ujumla.
Alibainisha kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kutengeneza mazingira ya upatikanaji haki na huduma ya msaada wa kisheria kwa kuondoa gharama za ada ya usajili wa usaidizi wa utoaji huduma ya msaada wa kisheria.
Aliongeza kuwa Serikali imeandaa mpango wa uandaaji wa vituo jumuishi vya sekta ya sheria ambavyo vitarahisisha utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi wote.
Pinda alisema kuwa katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara imetenga fedha kwa ajili ya utoaji wa msaada wa kisheria ikiwemo kazi za bodi ya ushauri ya msaada wa kisheria.
Ametoa rai kwa wajumbe wa kamati hiyo kuzingatia na kutekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa katika muongozo wa uundaji wa kamati za Mkoa pamoja na kushirikiana na jamii katika kupinga unyanyasaji wa wanawake na watoto kwa kuhakikisha waathirika wanapata haki stahiki.
Amewasisitiza wadau wa sheria kuandaa vitabu vyenye sheria ndogondogo kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuwezesha jamii kuelewa sheria mbalimbali kwa urahisi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makondo alisema kuwa Sheria ya msaada wa kisheria ilipitishwa rasmi mwaka 2017 na 2018 ambapo hadi sasa ni takribani miaka 5 tangu imeanza kutumika nchini.
Alieleza kuwa lengo la Wizara ni kusimamia na kuratibu watoa huduma za msaada wa kisheria nchini kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo bure na kwa viwango vinavyotakiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Phillipo Beno ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kutoa elimu juu ya upatikanaji na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria ambayo itawasaidia wananchi kupata haki zao pale inapohitajika.
Akiwakilisha wajumbe wa kamati ya utoaji huduma za msaada wa kisheria Mkoani Ruvuma, Shekhe Songambele ameipongeza Serikali kwa kutenga kitengo maalumu kinachotoa msaada wa kisheria kwa kuzingatia misingi ya kidini hasa katika kupambania haki za wanawake na watoto pamoja na mirathi.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa