BENKI ya NMB imechangia jumla ya viti 50 na meza 50 kwa ajili ya shule ya sekondari Narwi na kompyuta tano kwa ajili ya shule ya sekondari Rwinga zilizopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.
Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo imefanyika katika shule ya sekondari ya Narwi ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Sophia Kizigo.
Akizungumza katika hafla hiyo Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Janeth Shango amesema vifaa vyote vilivyotolewa katika shule hizo vimegharimu shilingi milioni tano.
“NMB tumeamua kushirikiana na shule hizi za Narwi na Rwinga ili kuwa jirani na jamii inayotuzunguka,kompyuta tulizozitoa katika shule ya sekondari ya Rwinga zitasaidia kuimarisha somo la TEHAMA’’,alisema Shango.
Hata hivyo Meneja huyo wa NMB Kanda ya Kusini amesema Benki hiyo imekuwa inapokea maombi mengi ya kuchangia miradi ya jamii na kwamba NMB imejikita zaidi katika maeneo ya elimu,afya na misaada ya hali na mali katika nyakati ngumu za majanga.
Kulingana na Shango,Katika kipindi cha mwaka 2018,NMB ilitenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii hali iliyosababisha Benki hiyo kuwa ya kwanza kuchangia maendeleo kuliko benki yoyote nchini.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Sophia Kizigo ameishukuru na kuipongeza Benki ya NMB kwa kuwajali wateja wake hali ambayo inadhihirisha kwa vitendo kuwa Benki hiyo ipo jirani ya jamii.
“Katika wilaya yetu ya Namtumbo karibu watumishi wote,fedha za tumbaku,korosho na mazao mengine yote,fedha zao zinapitia Benki ya NMB kutokana na huduma bora zinazotolewa na Benki hiyo’’,alisema Kizigo.
Amesema licha ya msaada wa madawati na kompyuta walizotoa,NMB pia wamekuwa wanachangia huduma mbalimbali za elimu na afya katika wilaya hiyo ikiwemo mradi wa ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Namtumbo ambayo Benki hiyo imekuwa inachangia kila mwaka katika hatua za mradi huo.
Hata hivyo Kizigo amesema wilaya hiyo inaanzisha kampeni mpya kuanzia mwaka huu ya ujenzi wa mabweni katika shule zote 30 za sekondari za serikali,hivyo ametoa rai kwa uongozi wa NMB kuendelea kuichangia miradi hiyo itakapoanza kutekelezwa.
Awali Mkuu wa Shule ya sekondari ya Narwi, Monica Kayombo akitoa taarifa kabla ya kukabidhiwa viti na meza 100,ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo ambao amesema umepunguza changamoto ya madawati katika shule hiyo.
Kayombo amesema shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2009 ina wanafunzi 404 wanaosoma kidato cha kwanza hadi cha nne na kwamba shule hiyo ina meza na viti 200 kati ya 404 zinazohitajika na kwamba shule ina madawati 48 huku upungufu ukiwa ni madawati 108.
Naye Mkuu wa shule ya sekondari ya Rwinga Suleiman Mohamed Alawi ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada wa kompyuta tano ambazo amesema zitasaidia kutatua changamoto ya gharama kubwa ya uchapaji wa mitihani ya ndani ya shule na mitihani ya ujirani mwema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Dani Nyambo amesema anatambua mchango mkubwa unaofanywa na Benki ya NMB katika wilaya hiyo na kusisitiza kuwa mchango wa viti na meza 100 na kompyuta tano utasaidia wanafunzi kuimarika katika teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo imeifanya dunia kuwa kijiji kimoja.
Yusufu Mwambe ni Diwani wa Kata ya Rwinga ambaye shule mbili za Narwi na Rwinga zilizopo katika Kata yake zimefaidika na msaada wa Benki ya NMB,ameshukuru kwa niaba ya wananchi na wanafunzi wa kata hiyo kwa msaada mkubwa ambao umepunguza changamoto zilizokuwa zinazikabili shule hizo.
“NMB wanafanya biashara hivyo kusema tu ahsante kwa maneno haitoshi,nawaomba wananchi wote wa kata yangu na watanzania kwa ujumla tuseme ahsante kwa kufungua akaunti katika Benki ya NMB’’,alisisitiza Mwambe.
NMB ndiyo Benki inayoongoza nchini kwa kufika wilaya zote nchini kwa asilimia 100,ina matawi zaidi ya 228,ATM zaidi ya 800,wakala wa NMB zaidi ya 6,000 na idadi ya wateja zaidi ya milioni tatu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Serikalini
Februari 13,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa