Benki kuu ya Tanzania( BOT) kwa niaba ya Serikali zote mbili yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huuza Dhamana za Serikali ikiwa ni njia ya kukopa fedha kutoka kwa taasisi mbalimbali na mwananchi mmoja mmoja.
Kauli hiyo imetolewa na kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Jeremiah E. Sendoro akiwakilishwa na Afisa Kilimo Mkoa wa Ruvuma Enock Ndunguru katika semina ya uwekezaji katika masoko ya fedha iliyotolewa na Benk kuu ya Tanzania (BOT) iliyo shirikisha watumishi wa umma, wadau wa taasis za fedha, na wananchi mbalimbali iliyofanyika katika ukumbi wa Songea Club tarehe 11 Novemba 2020.
Naye mwezeshaji kutoka Benki Kuu ya Tanzania ( Dar es saalam) Fidelis Mkatte alisema “Dhamana za Serikali za muda mrefu ni dhamana zinazoiva katika muda unaozidi mwaka mmoja, hata hivyo dhamana hizo za Serikali za muda mrefu kwa kiwango kikubwa huiwezesha Serikali kugharamia kwa muda nakisi katika bajeti yake inayosababishwa na upungufu wa mapato ukilinganisha na matumizi ya Serikali”.
Dhamana hizo huuzwa kwenye soko la awali kwa njia ya ushindani kupitia minada na baada ya hapo uuzaji wa dhamana hizo hufanywa kwenye soko la upili. Pia kiwango cha chini cha kuwekeza kwenye dhamana za Serikali za muda mrefu ni shilingi milioni moja 1,000,000 zikiwa katika mafungu ya shilingi laki mojamoja 100,000.
Aidha, Mpango huu hutolewa kupitia kwenye magazeti na hupatikana kwenye tovuti ya Benk kuu ya Tanzania; www.bot.go.tz, ukiwa unaonyesha dhamana ya Serikali itakayotolewa na tarehe yam nada.
Faida kwa mwekezaji ni Kuwekeza katika dhamana za Serikali ambazo ni salama kwani Serikali haitarajiwi kukiuka mategemeo ya wadai wake wakati wa malipo, Dhamana za Serikali zinahamishika, hivyo mwekezaji anaweza kuziuza kabla ya muda wake wa kuiva endapo itakuwa ni lazima afanye hivyo. Dhamana za Serikali zinaweza kutolewa kama dhamana kwa ajili ya mkopo pamoja na dhamana za Serikali kuwa na kiwango cha faida inayoridhisha”.
Akizita faida kwa upande wa Serikali ni Kugharamikia upungufu wa kibajeti (T-bills), Kupata fedha za kuendesha Miradi ya Maendeleo (T-bonds), Kusimamia Ujazo wa Fedha katika Uchumi, pamoja na kusaidia kusimamia mfumuko wa bei.
Aliwaasa walishiriki wa mafunzo hayo kuanza kuwekeza fedha zao katika masoko ya fedha ili waweze kunufaika na huduma hizo kwa kwenda tawi lolote la Benki kama CRDB na atapewa fomu ya maelekezo ya taratibu zote za uwekezaji wa masoko ya fedha ambapo kima cha chini ni tzs 500,000 kwa dhamana za muda mfupi na tzs 1,000,000 kwa dhamana za muda mrefu .
Alifafanua katika kuandaa muungozo huo, mambo yafuatayo yalizingatiwa ikiwemo na Dhamana zinazoiva, Ukopaji mpya, na Malengo katika kusimamia ujazo wa fedha kwenye mzunguko. Alisema “ KODI YA ZUIO” kwa Wawekezaji katika Dhamana za Serikali za Muda Mfupi pamoja na Dhamana za Serikali za Miaka 2 hulipa kodi ya zuio (10%) katika mapato yatokanayo na uwekezaji wao.
Wawekezaji katika Dhamna za Serikali za Miaka 5, 7, 10, 15 na 20 hawalipi kodi ya zuio. Hii ni katika kuhamisisha uwekezaji katika Dhamana za Serikali kwa Muda Mrefu ambazo huwa bora Zaidi kwa Serikali (Mkopaji). Alisisitiza Mkatte.
Dhamana zinazoiva, hulipwa kwa kutumia Dhamana zinazotolewa upya, na kiwango kinachopatika Zaidi ya mahitaji ya kulipa Dhamana zinazoiva huhesabika kama ukopaji mpya. Pia ingawa gharama za kulipia Dhamana zinazoiva hutokana na ukopaji mpya, faida wanayostahili kulipwa wawekezaji hulipwa kutokana na mapato ya ndani ya Serikali.
Mwisho alisema, Uwepo wa Dhamana za Serikali imekuwa chachu kubwa katika kufanikisha malengo mbalimbali ya serikali ikiwemo na Benki Kuu kufanikiwa kusimamia mfumuko wa bei, Serikali kufanikiwa kukopa kwa gharama nafuu katika riba za soko (competitive rates) na kupata fedha kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya ki-bajeti pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa jamii.
IMETAYARISHWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
13 Novemba 2020.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa