Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
02.12.2021
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imesaini nyongeza ya mkataba wa utendaji kazi na usimamizi wa shughuli za lishe kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia tarehe 01 Julai 2021 hadi tarehe 30 Juni 2026 kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya utapiamlo katika jamii.
Mkataba huo umesainiwa leo tarehe 02 Disemba 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea pamoja na watendaji wa kata ambao ni watekelezaji wa mkataba huo katika ngazi ya jamii, ambapo zoezi hilo limefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni katika utekelezaji wa kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani mnamo mwaka 2017 kutokana na kukithiri kwa hali duni ya lishe na udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 nchini ambapo aliagiza kuwepo kwa mkataba wa usimamiaji wa utekelezaji wa shughuli za lishe kati ya ofisi ya Makamu wa Rais na wakuu wa Mikoa yote 26 ndani ya Tanzania bara.
Akibainisha lengo la kusaini mkataba huo, Mgema alisema kuwa mnamo tarehe 24 Septemba 2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma iliingia mkataba wa utendaji kazi na usimamizi wa shughuli za lishe na Wakuu wa Wilaya zote 5 zilizopo ndani ya Mkoa wa Ruvuma ambapo mkataba huo umekuwa ukitekelezwa kwa muda wa miaka mitatu kuanzia tarehe 25 Septemba 2018 hadi tarehe 30 Juni 2021.
Mgema aliongeza kuwa tangu kusainiwa kwa mkataba huo ,ofisi ya Mkuu wa Mkoa na wadau wengine wa lishe walifanya tathimini sita na kubaini kuwa shughuli za lishe ni mtambuka na endelevu ambapo utekelezaji wa mkataba huo ulisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la utapiamlo katika jamii.
Alisema kuwa kwa kuzingatia umuhimu na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa awamu ya kwanza, pande zote mbili zilikubaliana kuongeza muda wa utekelezaji wa mkataba huo kwa sababu hakutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye maeneo mahususi yanayotekelezwa na mamlaka ya Serikali za mitaa na hivyo kutoathiri viashiria vingi katika mkataba wa lishe wa awali.
Kwa upande wake Afisa lishe Manispaa ya Songea Florentine Kissaka amewataka watendaji wa kata kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa nyongeza ya muda wa mkataba wa lishe katika ngazi ya jamii ili kuhakikisha elimu ya lishe inamfikia kila mwananchi na hatimaye kuondoa kabisa changamoto ya udumavu na utapiamlo.
Kissaka alibainisha kuwa katika kipindi cha Julai-Septemba 2021 hali ya utapiamlo na udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano imefikia kiwango cha asilimia 0.1% ambapo miongoni mwa yaliyochangia kushuka kwa kiwango cha watoto wenye utapiamlo ndani ya Manispaa ya Songea katika utekelezaji wa mkataba wa lishe ni pamoja na usimamizi mzuri wa viongozi kuanzia ngazi ya Wilaya, Halmashauri, kata na mitaa.
Aliongeza kuwa miongoni mwa changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa awamu ya kwanza ni pamoja na kiwango kidogo cha utambuzi wa watoto wenye utapiamlo katika jamii na baadhi ya kata kuchelewa kuleta taarifa ya utekelezaji wa mkataba katika maeneo yao kwa wakati.
Ametoa wito kwa watendaji wa kata kuongeza wigo wa kufanya uchunguzi wa hali ya lishe ili kuweza kuibua watoto wengi Zaidi wenye tatizo la udumavu na utapiamlo pamoja na Halmashauri kutoa motisha kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kuimarisha usimamizi kwenye ngazi ya kata na mitaa ambako ndiyo kiini cha kuleta mabadiliko katika jamii.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa