SERIKALI imedhamiria kuitumia nyotamkia(kimondo) iliyoanguka katika Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe kuutangaza utalii wa Tanzania baada ya kubainika kivutio hicho ni adimu duniani.
Moja vivutio adimu vya utalii vinavyowashangaza wengi ni nyotamkia (kimondo) ambayo iliyochomoka toka Sayari ya Jupiter mwaka na kuanguka mwaka 1840 katika kijiji cha Ndolezi Wilaya ya Mbozi ni moja ya kivutio kinachowashangaza wengi.
Nyotamkia hiyo ina uzito wa tani 12 ikiwa ni ya nane kwa ukubwa duniani kati ya nyotamkia zaidi ya 600 zilizoanguka toka angani sehemu mbalimbali ulimwenguni.
Utafiti unaonesha kuwa nyotamkia hiyo inaongoza kwa ubora ukilinganisha na nyotamkia zilizoanguka sehemu mbalimbali duniani.Nyotamkia au kimondo cha Mbozi kina madini ya chuma kwa zaidi ya asilimia 90.
Nyotamkia ya Mbozi katika historia ya nyotamkia zilizoanguka duniani haikubahatika kushuhudiwa na mtu yeyote wakati inashuka toka kwenye obiti yake angani kuja duniani mwaka 1840.
Hata hivyo kinachowavutia wengi ni kwamba nyotamkia hii ilikuja kuonekana tayari ikiwa imeanguka chini wakati wa utawala wa Mjerumani mwaka 1930 ambapo watalaamu wa kijerumani mwaka 1931 walikata kipande cha nyotamkia hiyo na kukipeleka nchini Ujerumani ili kukifanyia utafiti.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligissu anasema nyotamkia hiyo baada ya kupimwa ilionesha ina urefu wa mita tatu,unene wa mita 1.12,upana mita moja,ina uzito wa tani 12, nyotamkia hiyo iligundulika kuwa na aina tano za madini mbalimbali huku sehemu kubwa yakiwa ni madini ya chuma.
Anayataja madini yaliyomo katika nyotamkia hiyo kuwa ni chuma kipo kwa asilimia 90.45,madini ya nikel asilimia 8.66, shaba asilimia 0.69,sulfa asilimia 0.11 na madini ya fosiforasi ni asilimia 0.11.
“inaaminika kuwa nyotamkia ya Mbozi ndiyo ya kwanza kwa ubora duniani ukilinganisha na nyotamkia nyingine zilizoanguka duniani ambazo asilimia kubwa ni mawe na uzito wa kuanzia kilo tano tu’’,anasisitiza Maligisu.
Utafiti umebaini nyotamkia ya Mbozi ndiye pekee yenye madini ya aina tano wakati nyotamkia nyingine ikiwemo iliyoanguka nchini Afrika ya kusini ina uzito wa tani 60 na ya nchini Uingereza ina tani 30 lakini nyota hizo hazina ubora wowote wala madini,zaidi ya kuwa ni mfano wa jiwe linalopasuka kirahisi hali ambayo inasababisha watalii kutoka kona zote kutembelea zaidi nyotamkia ya Mbozi.
Makala hii imeandaliwa na
Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 11,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa