WANAWAKE waliopoteza matiti kutokana na kuugua saratani, watafanyiwa upasuaji wa kibingwa wa kurudishia tena kiungo hicho.
Upasuaji huo unaojulikana kitaalamu kama ‘Breast reconstruction after mastectomy’ utafanywa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).
ORCI ipo katika maandalizi ya kufikia hatua hiyo ya upasuaji wa kibingwa ikiwa ni moja kati ya makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Saratani ya China (Chinese Academy of Medical Science – Cancer Hospital (CAMS – CH)).
Makubaliano hayo yalisainiwa hivi karibuni mjini Beijing, China na Mkurugenzi wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage na Mkurugenzi wa CAMS – CH, Dk. Jie He, yalishuhudiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Dk. Mwaiselage alisema saratani ya matiti ni miongoni mwa saratani zinaozoongoza kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaopokewa na kuhudumiwa hospitalini hapo.
“Hivyo, tutashirikiana na wataalamu wenzetu kutoka katika taasisi hiyo upande wa upasuaji wa saratani hii. Ikigundulika mapema si lazima kutoa titi lote, tunaweza kutoa ule uvimbe uliopo pale na kuacha titi, lakini lazima uwe na mashine za kisasa za kutoa tiba mionzi (LINAC) ambazo tayari tunazo.
“Hata tukilitoa titi lote, tunatoa kutokana na upasuaji ambao unakuwa ni bora zaidi katika utoaji wa tiba hiyo, lakini baada ya upasuaji huo wa kuliondoa titi, kuna upasuaji unaofuata ‘breast reconstruction surgery’ (tiba ya kupandikiza titi).
“Kupitia makubaliano ya ushirikiano huu, tunakusudia wataalamu wa taasisi hiyo waje nchini ili kuwajengea uwezo wataalamu wetu wa ndani, jinsi gani ya kutoa huduma hiyo kwa usahihi,” alisema.
Alisema titi ni kiungo muhimu kwa mwanamke na linapotolewa humwathiri kisaikolojia na sasa kupitia makubaliano hayo wataanza kutoa huduma hiyo.
Dk. Mwaiselage alisema pia kutakuwa na mafunzo ya juu kwa madaktari bingwa wa saratani (super specialization).
Kwamba wataalamu kutoka China watakuwa wakija nchini kuwafundisha kwa vitendo wataalamu wa ndani kwa kila saratani husika hasa zile zinazoongoza nchini.
Alisema wamekubaliana pia taasisi hiyo itoe mafunzo ya muda mrefu kwani Tanzania inakabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa, hasa kwa upande wa magonjwa ya saratani kwa upasuaji.
“Lakini kwa kuwa ORCI hatufanyi upasuaji, tumelenga kwamba madaktari watakaokwenda kujifunza mafunzo hayo watatoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas-Mloganzila),” alisema.
Alisema pia wamekubaliana kufanya tafiti kwa pamoja na wamelenga zitasaidia katika kuimarisha huduma za kinga na tiba dhidi ya magonjwa hayo.
CHANZO NI MTANZANIA
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa