OFISI za vijiji 12 wilayani Songea mkoani Ruvuma zimenufaika na msaada wa mbao za matangazo kwa ajili ya kubandika matangazo na taarifa mbalimbali ikiwemo ya mapato na matumizi pamoja na miradi ya maendeleo kwa lengo la kuongeza uwazi katika ngazi za vijiji wanavyofanyia kazi.
Msaada huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na mkurugenzi mkuu wa asasi isiyo ya kiserikali ya Millenium Arts Group Mnung'a Shaib Mnung'a kupitia ufadhili wa The Foundation For Civil Society(FCS)ya Jijini Dar es salaam kwenye kongamano la ushawishi na utetezi juu ya masuala ya utawala Bora lililofanyika katika kata ya Magagura wilayani humo.
Mnung'a alivitaja vijiji vilivyonufaika na msaada wa mbao hizo za matangazo kutoka katika kata nne ambazo zimepitiwa na mradi wa utawala Bora kuwa ni Lusonga,Masangu,Kizuka,Magagura,Mbilo,Ngahokola,Litapwasi,Uyahudini,Lihangweni,Lipaya,Mpitimbi A na Mpitimbi B vyote vya wilayani Songea
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo kwa wenyeviti wa vijiji hivyo,mkurugenzi huyo aliwataka viongozi hao kutumia mbao hizo za matangazo kwa ajili ya kubandika matangazo na taarifa mbalimbali za mapato na matumizi kwa ajili ya kuondoa manung'uniko na migogoro baina ya viongozi na wananchi.
Aidha amewataka wenyeviti hao kuzingatia misingi ya utawala Bora ikiwa pamoja na uwajibikaji,uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga,kutekeleza na kufanya ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa madai kuwa kuto kufanya hivyo kutapelekea wananchi kutokuwa na Imani na viongozi wao na kuwavunja moyo wa kujitolea katika shughuli za maendeleo.
Alisema kuwa miradi mingi ya maendeleo vijijini inakwama na mingine kutekelezwa chini ya kiwango kutokana na baadhi ya wenyeviti wa vijiji na watendaji wa kata kutoshirikisha wananchi na matokeo yake huzuka migogoro na malumbano kati ya viongozi na wananchi jambo ambalo linapelekea kukwamisha shughuli za maendeleo.
Akiongea kwa niaba ya wenyeviti wenzake,mwenyekiti wa kijiji cha Ngahokola wilayani Songea Eneck Haule ameipongeza na kuishukuru asasi hiyo kwa kutoa msaada huo kwa madai kuwa awali ofisi nyingi za vijiji hazikuwa na mbao hizo jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mahojiano toka kwa wananchi na kuamsha hali ya kujitolea.
Mwandishi ni Julius Konala wa Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa