Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango atakayeshughulikia sera Adolf Hyasinth Ndunguru na Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Rais Magufuli ameitaka TRA na Wizara ya Fedha na Mipango kupanua uwigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi na kuibua vyanzo vipya vya mapato, pamoja na kujenga mazingira rafiki kwa watu wengi zaidi kulipa kodi ili kuongeza makusanyo ya kodi.
Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji wa TRA ambayo mpaka sasa inakusanyaji kodi kwa walipa kodi Milioni 2 na Laki 7 tu kati ya Watanzania wote zaidi ya Milioni 55, na amesema kwa mtindo huo TRA itakuwa inazidi kuwakamua walipa kodi wachache wakati ingeweza kupanua uwigo wa kodi na kuweka viwango vya kodi vinavyolipika na vitakavyowavutia watu wengi zaidi kulipa kodi.
“Ukienda mipakani wafanyabiashara wanafungua maduka upande nchi za wenzetu na sio upande wa Tanzania, na sababu ni kwamba wakifungua upande wa Tanzania wanasumbuliwa na TRA, wekeni viwango vya kodi vinavyolipika ili watu wengi waweze kulipa kodi badala ya kukwepa” Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na mrundikano wa kesi za kodi mahakamani na ametaka tatizo hilo lifanyiwe kazi kwa kuwa linasababisha kodi nyingi kutolipwa kwa kusubiri mivutano ya kesi.
Amempongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji kwa ufuatiliaji mzuri wa fedha za bajeti zinazoelekezwa katika miradi mbalimbali na kuchukua hatua zinazostahili ikiwemo kuzirejesha hazina na kuzielekeza mahali pengine zinapohitajika.
Aidha, Rais Magufuli amemtaka Naibu Katibu wa Fedha na Mipango Mkuu Ndunguru na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mbibo kwenda kurekebisha dosari zote zilizopo katika ofisi zao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watumishi wanaoonekana kuwa kikwazo cha kutekeleza mipango ya Serikali.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema viongozi hao wanatarajiwa kufanya vizuri zaidi katika nafasi walizopewa hivi sasa hasa ikizingatiwa kuwa wanakwenda kufanya kazi katika ofisi zenye mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Nae Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere wamemshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi wa viongozi hao na wameahidi kwenda kusimamia kwa ukaribu zaidi utekelezaji wa fedha za bajeti na kufanyia kazi changamoto ya kupanua uwigo wa kodi na kuongeza idadi ya walipa kodi
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa