Chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) ni chama kinachoundwa na wafanyakazi/Wanachama kutoka katika Halmashauri za Majiji na Idara zake, Halmashauri za Manispaa na Idara zake, Halmashauri za Wilaya na Idara zake, mashirika ya maendeleo ya Uchumi, Mifuko ya Pensheni (PSSSF) na mamlaka nyingine zingine za ajira. Ambapo wanachama wa TALGWU toka mamlaka hizo hulindwa na kutetewa maslahi yao kwa mujibu wa kanuni za Nchi.
Hayo yametamkwa na Katibu wa TALGWU Mkoa wa Ruvuma Ashraffu Chussi kwenye mkutano wa TALGWU Mkoa wa Ruvuma uliofanyika tarehe 26 juni 2021 katika ukumbi wa AJUCO Manispaa ya Songea na kuhudhuliwa na Mh. Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), wajumbe zaidi ya 237 kutoka kwenye matawi 79 Mkoani Ruvuma, viongozi mbalimbali ngazi ya mkoa, pamoja na Msimamizi wa Uchaguzi kutoka Idara ya Kazi Mkoa wa Njombe kwa lengo la kufanya chaguzi za vingozi ngazi Mkoa na wawakilishi Mkutano mkuu Taifa.
Chussi alisema Katiba ya Chama cha TALGWU toleo la 2016 Ibara ya 5.10 inayoelekeza kufanyika kwa Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa za kazi kwa kipindi cha miaka (5) 2016-2021 na kufanyika chaguzi za viongozi wa nafasi mbalimbali ambapo siku ya pili 27 juni 2021 baada ya uchaguzi kufanyika wajumbe wote walipata semina ya utawala bora, na matumizi ya fedha za Chama.
Alisema TALGWU Mkoa wa Ruvuma ina wanachama 2859 kati ya watumishi wasio walimu 3792 sawa na 75% ya watumishi wote wasio walimu katika mkoa wa Ruvuma. Akizitaja changamoto zinazowakabili wanachama Mkoani Ruvuma ni pamoja na watumishi kutolipwa madeni ya uhamisho, likizo, matibabu na malimbikizo ya mishahara, Wakurugenzi Halmashauri kuhamisha watumishi bila kuwalipa stahiki zao kwa wakati kinyume na maelekezo ya serikali yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais, uchache wa watumishi sekta mbalimbali hasa Idara ya Afya pamoja na upungufu wa Vitendea kazi.
Mgeni Rasmi katika mkutano huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Wilbert Ibuge ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema ambaye alisema “kazi ya kiongozi ni kuonyesha njia, kutatua changamoto au kero za wanachama wake, kuwa wabunifu wa miradi ya maendeleo na kujiepusha na tamaa za fedha kwa maslahi ya chama”.
Pololet alisema, Awali vyama vya wafanyakazi vilikuwa na migomo mbalimbali katika kudai haki lakini kwa sasa vyama vya wafanyakazi wamekuja na utaratibu mpya wakutumia njia ya majadiliano na kukubaliana jambo kwa pamoja. Alisema hiyo ndiyo njia sahihi.
Akijibu Risala iliyosomwa na katibu wa chama hicho ambapo alisema Serikali imefanya mambo mengi sana na inaendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa watumishi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi pamoja kuongeza vitendea kazi kwenye vituo vya afya, vifaa tiba, dawa na vitenganishi vinatolewa kwa asilimia 98%.
Alibainisha kuwa kwa muda wa miaka 5 iliyopita Serikali imeanza kuboresha miundombinu ya afya Mkoani Ruvuma ambapo alisema vituo vya vya afya 15 na vingine vinajengwa ikiwemo na Halmashauri ya Nyasa kituo 1, Halmashauri ya wilaya ya Songea 1, na halamashuri ya wilaya ya Namtumbo vimekamilika na kutoa huduma ya awali ya OPD na baada ya kupokea vifaa huduma zote zitatolewa ikiwemo na upasuaji.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma umepokea milioni 500 kwa kila Hospitali kwa ajili ya kuongeza WOD za wanawake, wanaume na watoto. Pia Halmashauri ya Wilaya ya Songea imepokea shilingi milioni 900 kwa ajili ya kujenga vituo 2 vya afya Madaba na Mtyangimbole, pia Manispaa ya Songea imepokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya kituo cha afya Ruvuma, Shilingi milioni 400 Magagura, na shilingi milioni 400 Matimila.
Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote na makatibu Tawala wa Mikoa wahakikishe wanalipa madai ya likizo, uhamisho, malimbikizo kwa watumishi ambao wanadai na hadi kufikia ocktoba 30 2021 yawe yamelipwa. Alisema “Rais wa Nchi hii akiagiza hiyo ni sheria. Hata nyie watumishi mna haki ya kukataa kuhama kituo kimoja kwenda kituo kingine kama hujalipwa haki yako lakini mkizungumza kimahusiano hukatazwi”. Pololet alisisitiza.
Naye Rais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) ambaye pia ni Mwenyekiti wa TALGWU Taifa Tumaini Nyamhokya alisema wapo watumishi wanaolipwa mishahara kwa mapato ya ndani ambapo mishahara hiyo hulipwa bila kupeleka makato kwenye mifuko husika ambapo amewataka Waajiri wote kuhakikisha wanapeleka makato TRA, Mifuko ya jamii, mfuko wa TALGWU, pamoja na mfuko wa afya.
Mh. Rais Nyamhokya alisema miongoni mwa mafanikio ya chama kwa kushirikiana na TUCTA ni pamoja na kuwarudisha watumishi zaidi 8000 hususani wa darasa la 7 ambao waliondolewa kazini pamoja na kurudisha kikokotoo cha awali, na kupandisha madaraja kwa watumishi ambapo kuanzia julai 2021 kutakuwa na mabadiliko ya mishshara. Pia amewataka watumishi kuwa waaminifu kazini hususani wakusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia POS.
Naye Afisa kazi ambaye alikuwa Msimamizi wa Uchaguzi Albert Luka Ngendelo alisema utaratibu wa kupiga kura utafuata kanuni za Chama toleo la 2018, kanuni ya kwanza, kanuni ndogo ya 6 katika kifungu kidogo cha 6 inayozungumzia uchaguzi wowote wa chama utafanyika kwa kupiga kura ya siri. pia kanuni ndogo ya kwanza kanuni ndogo ya 7 aya ya 5 ambayo inasema uchaguzi wa kujaza nafasi nyingi za makundi, ushindi utahesabiwa kwa kupata wingi wa kura alizozipata muombaji kwa mujibu wa katiba.
Mwisho, Ngendelo alitangaza matokeo ya uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi kwa wagombea ambapo ngazi ya Mwenyekiti Mkoa mgombea alikuwa mmoja ambaye ni Wily Luambano ambaye alipigiwa kura za ndiyo/hapana ikiwa kura zilizopigwa ni 229, kura zilizoharibika 8, kura za hapana 27, na kura za ndiyo ni 194 kisha kumtangaza ndugu Wily David Luambano kuwa Mwenyekiti wa TALGWU Mkoa wa Ruvuma.
TALGWU CHAMA IMARA HUDUMA BORA KWA WANACHAMA
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
28 JUNI 2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa