Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Generali Wilbert Ibuge ameongoza kikao kazi cha kufanya tathimini juu ya utoaji wa huduma bora za afya kwa Mkoa wa Ruvuma, kikao kilichofanyika hapo jana tarehe 10 Juni 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Kikao ambacho kilijumuisha wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma, Wakurugenzi wa Halmashauri 8, Wenyeviti wa Halmashauri Pamoja na viongozi mbalimbali, kwa lengo la kujenga uelewa juu ya utoaji huduma bora za afya kwa jamii.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Generali Ibuge amesema kwamba lengo kuu la kuitisha kikao cha pamoja na viongozi wote ni kuongeza uelewa na uwajibikaji katika kusimamia sekta ya afya hususani upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya afya pamoja na ukusanyaji wa mapato kwa njia ya mfumo wa GOTHOMIS.
Ibuge amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kupitia Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma kuwasilisha taarifa ya kila robo mwaka kuhusiana na hali ilivyo katika utoaji wa huduma za afya kwa Mkoa wote wa Ruvuma pamoja na kuainisha changamoto mbalimbali ambazo zinajitokeza hasa katika Nyanja ya upatikanaji wa dawa na ukusanyaji wa mapato ili kuweza kukabiliana nazo na kuleta maendeleo katika sekta ya afya Mkoani Ruvuma.
Pia ametoa maagizo kwa viongozi hao, ifikapo septemba mosi 2021 vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya umma katika Mkoa wa Ruvuma viwe vimefungwa mfumo wa kukusanya mapato kwa njia ya kidigitali GOTHOMIS, na yeyote atakayeshindwa kutii agizo hilo hatua kali zitachukuliwa.“Ibuge alisisitiza”
Ibuge aliongeza kuwa mapato na matumizi ya vyanzo vyote katika Halmashauri zote yawe yanajadiliwa kwenye vikao vya kisheria na kamati za ndani ya Halmashauri, na kuhakikisha ukusanyaji wa mapato katika sekta afya ufikie asilimia 80% ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa dawa katika vituo vya afya.
Aliongeza kuwa kila Halmashauri ihakikisha wanahamasisha jamii kujiunga na mfuko wa huduma ya afya ya jamii ulioboreshwa iCHF ambapo mpaka sasa Mkoa Ruvuma umesajili kaya 18,039 ambayo ni sawa na asilimia 5% kati ya kaya 12,203 ambayo ni sawa na asilimia 3.4% zilizopo hai, na kaya 5,851 sawa na asilimia 1.6% ni kaya mfu.
Naye Mfamasia Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Shaloon Peter amesema hadi kufikia mwezi Mei 2021 Mkoa wa Ruvuma umepata jumla ya Tshs. 3,752,463,234.89 ambayo ni sawa na asilimia 80.1% kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya ambapo katika fedha hizo Mkoa umetumia Tshs. 1,530,397,382.84 ambayo ni sawa asilimia 40.78%.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA;
11.06.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa