Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
15.02.2022
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Balozi Wilbert Ibuge amezindua rasmi zoezi la uwekaji wa anuani za makazi huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa viongozi wanaosimamia zoezi hilo.
Ibuge amezindua mpango huo hapo jana Februari 14, 2022 katika eneo la NMB Bank lililopo Manispaa ya Songea ikiwa ni siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutoa maagizo kwa wakuu wa Mikoa nchini kusimamia mpango huo kikamilifu.
Akizungumza kabla ya kuzindua mpango huo, Ibuge alisema kuwa mfumo wa anuani za makazi ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa na hivyo ni lazima kila kiongozi ajitoe katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa kwa muda maalumu uliopangwa na serikali.
Alisema utekelezaji wa mpango wa uwekaji wa anuani za makazi na posti kodi unagharamiwa na Serikali kwa shilingi bilion 28 ambapo kwa mujibu wa maagizo ya Rais yaliyotolewa Februari 8, 2022 amewataka wakuu wote wa Mikoa kusimamia zoezi hilo ili ifikapo mwishoni mwa mwezi Mei 2022 liwe limekamilika, ikiwa kwa Mkoa wa Ruvuma zoezi imeadhimiwa kukamilika ifikapo Aprili 31, 2022. “Alibainisha”
Amewataka wakuu wa Wilaya, wakurugenzi pamoja na viongozi wa ngazi zote kujipanga kikamilifu ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wananchi katika kutekeleza zoezi hili bila kuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi.’Alisisitiza’
Ametoa rai kwa wananchi wote Mkoani Ruvuma kushiriki kikamilifu kuelekea zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajia kufanyika mwezi Agosti mwaka huu kwa lengo la kupata idadi kamili ya watu itakayosaidia katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa wananchi.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Steven Ndaki alieleza kuwa chimbuko la uwekaji wa anuani za makazi ni utekelezaji wa sera ya Posta ya mwaka 2003, ambayo inazitaka nchi wanachama kuanzisha mfumo wa anuani za makazi na posti kodi kwa mujibu wa sheria za Serikali za mitaa; mamlaka ya mji sura ya 247 ambayo imetoa mamlaka ya kuzipa majina barabara na kutoa namba kwenye nyumba za wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema, akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya Mkoani Ruvuma alisema kuwa wamejipanga kusimamia na kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi kwa kufuata miongozo na taratibu zilizotolewa na Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alisema zoezi hilo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea litafanyika katika kata 21, mitaa 95, barabara zilizo chini ya TARURA 403 pamoja na nyumba elfu 64,906 ambazo zimehesabiwa kwa mujibu wa taarifa ya awali iliyotolewa ambapo ameahidi kusimamia zoezi hilo kikamilifu na kwa wakati.
Uzinduzi huo ulihitimishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kukabidhi kibao cha anuani ya makazi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea pamoja na kuweka rasmi kibao kuonyesha jina la barabara iliyopo Manispaa ya Songea yenye jina NMB Bank Songea, 2 barabara ya NMB, 57101 Songea Ruvuma ikiwa ni kiashiria cha uzinduzi wa zoezi la uwekaji anuani za makazi na posti kodi.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa