viongozi Mkoani Ruvuma wanatakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ya kujikinga dhidi ya ugonjwa hatari wa CORONA ikiwemo na kuchukua tahadhari kwenye maeneo ya Mikusanyiko mbalimbali kwa kuhakikisha wananchi wanachukua tahadhari kwa kunawa mikono kwa maji tiririka, kutumia vitakasa mikono, pamoja na kuvaa barakoa.
Ibuge ametoa rai kwa wananchi Mkoani humo kufuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa Afya ili kujikinga na wimbi la tatu la ugonjwa hatari wa CORONA ambapo alisema Mkoa wa Ruvuma bado haujawa tishio kwasasa, bali amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwani kujikinga ni bora kabla ya kuugua.
Hayo yamebainishwa katika kikao kazi cha watumishi wa Sekta ya Ardhi Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea tarehe 13 julai 2021 ambapo mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, kilichohudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi kutoka Halmashauri 8, pamoja na maafisa Tawala Wilaya kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa kazi za ardhi kwa mwaka 2019 hadi 2020 na kuweka malengo ya mwaka 2021/ 2022 pamoja na mikakati ya utatuaji wa migogoro ya ardhi kwa wananchi.
Alisema, azma kuu ya Serikali ni kuboresha utendaji kazi, kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Sekta ya Ardhi nchini kwa kuondoa / kupunguza malalamiko kwa wananchi ikiwemo na kutoa huduma bora na kwa kuzingatia maadili ya kazi pamoja na Kutojihusisha na vitendo vya rushwa, sambamba na kuwatembelea wananchi katika maeneo yao badala ya kusubiri migogoro hiyo iwakute Ofisini.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Mipangomiji Namba 8 ya Mwaka 2007 Fungu la 7 kifungu kidogo cha (1), Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya ni Mamlaka za Upangaji (Planning Authorities), na kifungu kidogo cha (5) cha Sheria ambayo inaelekeza mambo muhimu yanayopaswa kufanywa na Mamlaka za Upangaji.
Ametoa wito kwa viongozi hao kuweka utaratibu wa kufanya vikao vya wataalamu wa ardhi mara kwa mara ili kubaini changamoto mbalimbali za wananchi na kuweka mpango mkakati wa utatuzi wa changamoto hizo. “Brigedia Ibuge alisisitiza”
Naye kamishna wa Ardhi Mkoa wa Ruvuma Ildefonce L. Ndemela alisema katika mwaka wa fedha 2020/2021, Ofisi ya ardhi Mkoa wa Ruvuma imesimamia na kutekeleza kazi za upangaji, upimaji, umilikishwaji, uthamini, usajili wa Hati na nyaraka mbalimbali, utatuzi wa migogoro ya Ardhi na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ambapo kwa mwaka wa Fedha 2020 / 2021, Mkoa wa Ruvuma ulipangiwa malengo ya kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 4.6 ambayo walikusanya kwa asilimia 87%, pia kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Mkoa umepangiwa malengo ya kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 3.0.
Ndemela alibainisha baadhi ya changamoto mkoani Ruvuma ni pamoja na Upungufu wa Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika baadhi ya Mabaraza yaliyopo Mkoa wa Ruvuma, Upungufu wa vitendea kazi kama printer, plotter na mashine ya kudurufu kwa baadhi ya Halmashauri kwa ajili ya kutengeneza Ankara za malipo pamoja, ilani za madai ya kodi pamoja na nyaraka zingine.
Katika kutatua changamoto hizo Mkoa wa Ruvuma umeweka mikakati ambayo ni pamoja na kuajiri watumishi wa kada ya ardhi, Kuhakikisha wadaiwa sugu wote wanapelekewa notisi za madai ya kodi na kuwafikisha mahakamani kwa wale ambao watakaidi kulipa kodi kwa wakati, Kufanya matangazo mbalimbali kwenye vyombo vya habari, kufanya matangazo ya kuzunguka mtaa kwa mtaa na kubandika vipeperushi vya kuwakumbusha wamiliki kulipa kodi ya pango la Ardhi, Kushirikiana na Wenyeviti na Watendaji wa Mitaa kusambaza ilani za madai ya kodi ya pango la Ardhi, Kushirikiana na Mamlaka za upangaji katika zoezi la upimaji pamoja na urasimishaji wa makazi holela, kwa ajili ya kuongeza viwanja vipya ili kuongeza milki mpya na makusanyo. “Ndemela Alibainisha”
AMINA PILLY;
AFISA HABARI- SONGEA MANISPAA;
14 julai 2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa