Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewataka wakuu wa Taasisi na Idara mbalimbali Mkoani Ruvuma kuweka utaratibu wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa lengo la kupunguza migogoro inayowakabili wananchi.
Hayo yametolewa katika kikao cha wakuu wa Taasisi na Idara mbalimbali Mkoani Ruvuma kwa lengo la utatuzi wa kero kwa wananchi kilichofanyika leo tarehe 14 aprili 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Mndeme alisema kila Kiongozi anatakiwa atimize wajibu wake wa kazi aliyopewa pamoja na utatuzi wa kero mbalimbali za wananchi ikiwemo na kero ya Maji, Umeme, Barabara, Miundombinu ya shule na Ardhi. Aliongeza kuwa endapo viongozi wataendelea kufanya kazi maofisini bila kwenda kwa wananchi kuibua kero zinazowakabili wananchi hao kutapelekea uwepo wa malalamiko mengi ambayo itapelekea kuyapeleka ngazi ya juu (Mkoani).
Aliongeza kuwa uwepo wa kero nyingi za wananchi huashiria kutojituma kwa viongozi waliopo katika nafasi zao za kazi ambapo viongozi hao wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kazi sambamba na kutatua kero za wananchi bila kusubiri viongozi wa Kitaifa watatue kero hizo.
Amewaagiza Wakuu wa Taasisi na Idara kuunda mkakati maalumu wa kutatua kero za wananchi kuanzia ngazi ya chini kwa kuweka utaratibu wakuratibu kero hizo kwenye rejista ambazo zitaonyesha aina ya kero, Idara husika na namna gani imetatuliwa na endapo itakua haijatatuliwa ipelekwe ngazi ya juu (Mkoa) kwa utatuzi Zaidi.
Alisema “Ukosefu wa mahusiano mazuri miongoni mwa viongozi, kutofanyika vikao vya kisheria na kutokuwa na matumizi mazuri ya Lugha kwa wananchi hupelekea kutokea kwa malalamiko/kero kwa wananchi”.
Amewaagiza Viongozi hao kuhakikisha kila ifikapo mwishoni mwa mwezi kufanya tathimini ya utekelezaji wa zoezi hilo la utatuzi wa kero kwenye Taasisi yake, uwasilishaji wa taarifa ya kero zinazohitaji utatuzi wa kisera, uandaaji wa rejista ya malalamiko ya wananchi, uundaji wa timu ndogo ya kuratibu na kutatua kero za wananchi pamoja na kikao cha tathimini cha majumuisho ya utekelezaji wa zoezi la utatuzi wa kero kila ifikapo robo ya mwaka. “Mndeme alibainisha”.
Mndeme amewataka wafanyabiashara Mkoani Ruvuma kuuza bidhaa/vyakula kwa bei rafiki katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani ili bidhaa za chakula zipatikane kwa urahisi kwa Waislamu wanaoshiriki kwenye mfungo wa Ramadhani.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho amewataka wataalamu kutekeleza wajibu wao ikiwemo utekelezaji wa agizo lililotolewa katika kikao cha RUWASA ambalo lilikuwa linahusu utatuzi wa kero ya maji kwa wananchi.
Oddo alisema kila mtaalamu anatakiwa kujituma katika nafasi yake ya kazi ili wananchi waweze kupata huduma thabiti inayotolewa na Serikali yao.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
14/04/2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa