Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
11.12.2021
Chama cha ushirika cha akiba na mikopo (SACCOS) Manispaa ya Songea chajipanga kutoa mafunzo kwa wanachama, watendaji na viongozi kwa lengo la kuongeza uelewa na ufanisi wa kazi katika chama hicho.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa SACCOS Manispaa ya Songea Amiry Ayoub katika mkutano wa 29 wa mwaka huu leo tarehe 11 Disemba 2021 uliofanyika katika ukumbi wa AJUCO Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, pamoja na wanachama wa chama hicho.
Amiri alieleza kuwa kwa mwaka 2021 chama hicho kimefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 613, 522, 000 kutoka kwenye makusanyo ya ndani ambapo katika fedha hiyo shilingi milioni 396, 850, 00 imetumika kutoa mikopo kwa wanachama 169.
Alisema kuwa miongoni mwa changamoto zinazokikabili chama hicho ni pamoja na baadhi ya wanachama kushindwa kurejesha mikopo yao kwa wakati, wanachama wanaochangia akiba kwa fedha taslimu kushindwa kuchangia kwa wakati pamoja na baadhi ya wananchama kuuza mikopo yao kwa Taasisi kubwa za kifedha hali inayopelekea chama kukosa mapato.’Alibainisha’
Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2022 chama kimejipanga kuongeza msukumo wa ukusanyaji wa hisa, akiba na hisa za hiari kwa lengo la kukuza mtaji wa chama kwa kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato ya chama hicho, kutoa huduma bora kwa wanachama kwa wakati kulingana na mwongozo pamoja na kuongeza wigo wa huduma ili kupata wananchama wengi Zaidi.
Kwa upande wake Meneja wa SACCOS Manispaa ya Songea Winifrida Komba alisema kuwa chama hicho kilianzishwa kwa lengo la kuwanufaisha kiuchumi wafanyakazi wote wa umma waliopo ndani ya Manispaa ya Songea ambapo hadi sasa chama hicho kimefanikiwa kujiendesha chenyewe kwa kupitia fedha zinazokusanywa kwa mapato yake ya ndani.
Naye Afisa ushirika Manispaa ya Songea Given Mariki ametoa rai kwa wanachama wote waliokopa fedha na kushindwa kurudisha kwa wakati kuhakikisha wanarudisha fedha hizo kabla ya hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Ametoa pongezi kwa bodi ya uongozi wa chama hicho kwa kufanikiwa kuongeza wanachama wapya 14 kwa mwaka 2021 na amewataka wafanyakazi ambao bado hawajajiunga na chama hicho kuchukua hatua kwa kujisajili ili kuweza kujiinua kiuchumi.
Wakizungumza kwa wakati tofauti wanachama wa chama hicho wamesema kuwa miongoni mwa faida ya kujiunga na SACCOS Manispaa ya Songea ni pamoja na kupata mkopo wa riba nafuu ambayo huwasaidia wanachama kutatua changamoto mbalimbali pamoja na kuipongeza bodi ya uongozi kwa usimamizi mzuri wa mapato ya chama na uwepo wa mikakati thabiti ya chama iliyowekwa.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa