MKUU wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Pololet Mgema amestushwa na taarifa zilizosambazwa jana Mei 20,2018 na Kituo cha Habari cha ITV,zinazohusu kufungwa kwa zahanati tatu katika wilaya hiyo kwa kukosa watumishi.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea,Mgema amesema Kituo hicho kimemnukuu Mfadhili kutoka nchini Ujerumani ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Misheni ya Peramiho Dk.Ansgar Stuffe kuwa katika vijiji vya Litisha,Mdunduwalo na Lugagala kuna zahanati zimefungwa kwa kukosa watumishi na zahanati moja kati ya hizo imegeuzwa duka.
Amesema taarifa hiyo ambayo pia imesambazwa na kurasa za mitandao ya kijamii ya ITV, imekosa ufafanuzi kuwa mfadhili huyo anazungumzia zahanati zipi ambazo zimefungwa kama zinazomilikiwa na misheni au serikali hali ambayo imesababisha upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii ambayo imeandika kuwa zahanati hizo ni za serikali jambo ambalo sio sahihi.
“Zahanati zetu zote katika vijiji hivyo ambavyo vimetajwa bado ujenzi wake haujakamilika na hazijaanza kutoa huduma,kwa hiyo haiwezekani zahanati au kituo ambacho hakijakamilika kujengwa,kiweze kufungwa kwa sababu ya kukosa watumishi’’,anasisitiza Mgema.
Ameongeza kuwa kituo ambacho kinaweza kufungwa kwa kukosa watumishi ni kile ambacho ujenzi wake ulishakamilika,kimepata usajiri na kimeanza kufanyakazi.
Kutokana na hali hiyo serikali wilayani Songea inakitaka Kituo cha ITV kukanusha taarifa hiyo kwa uzito ule ule kama kilivyotoa taarifa hiyo haraka iwezekanavyo.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 21,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa