Serikali itaendelea kusimamia matumizi sahihi ya stendi ya Mfaranyaki kama ilivyoamriwa kupitia vikao vya kisheria vya Baraza la Madiwani la Manispaa ya Songea, kwa ajili ya matumizi ya usafiri wa daladala na sio vinginevyo.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Songea Cosmas M. I. Nshenye katika kikao na Waandishi wa Habari kwa ajili ya kutoa tamko kwa wafanyabiashara wote na wenye vyombo vya usafirishaji kurudisha huduma zao ndani ya masaa 24 kilichofanyika leo 22 februari 2021 katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Songea.
Nshenye amesema ukiwa mfanyabiashara tayari utakuwa umeingia kwenye mkataba na Serikali pia mfanyabiashara yeyote anatakiwa kufahamu athari za mgomo zitakazotokea na wanaoathirika sio Serikali pekee bali kuna athari za kijamii, kiuchumi na nyinginezo.
Ameagiza Afisa wa LATRA “kufuta mara moja route ya mabasi yote yanayotoa huduma ya usafirishaji kuanzia Songea mjini hadi Mbinga Mjini na kwa mfanyabiashara yeyote mwenye nia ya kutoa huduma za usafirishaji abiria kutoka Songea Mjini hadi Mbinga Mjini aombe mara moja ili aweze kufanya shughuli za usafirishaji katika route hizo”. Pia Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa route nyingine ili kuona ufanisi wake katika kuhudumia wananchi. Nshenye amesisitiza.
Alisema Serikali ina taarifa kupitia vikao vilivyofanyika hivi karibuni vya wafanyabiashara kuwepo kwa matamshi ya lugha za matusi, uchochezi na uvunjifu wa Amani na kuhujumu mipango ya Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi.
Amewataka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi mara moja na kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa wahusika wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo, pamoja na kuweka Mpango mbadala wa haraka wa utatuzi wa suala la usafiri katika kurudisha huduma za usafiri.
Ametoa agizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea na LATRA kuwachukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria za Leseni ikiwepo kuwanyang’anya Lesen za biashara wahusika wote watakaokaidi maelekezo ya kurudi kazini/ kufungua biashara zao ndani ya masaa 24 toka tamko hili limetolewa.
Mwisho aliwashukuru wananchi na wadau wote kwa utulivu mkubwa katika kipindi hiki ambacho Serikali imeendelea kushughulikia changamoto pamoja na wadau walioendelea kutoa huduma na kupuuza matamko yaliyotolewa na watu wasiokuwa na nia njema na Serikali yao.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
22.02.2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa