SHULE ya sekondari ya wavulana Songea (Songea boys) iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,imepokea jumla ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matano yakiwa ni maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Elimu Sekondari katika Manispaa hiyo, Devota Luwungo,Bodi ya shule ya sekondari hiyo Juni 21 imepewa mafunzo elekezi na kusisitiza kuwa ujenzi wa madarasa hayo unaanza mara moja.
Amesisitiza kuwa hadi kufikia Agosti 15 mwaka huu,wanatarajia ujenzi wa madarasa hayo utakuwa umekamilika na kwamba hivi sasa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano katika shule za sekondari za serikali zilizopo katika Manispaa ya Songea.
Anazitaja shule za sekondari za serikali za kidato cha tano ambazo zinapokea wanafunzi kuwa ni Songea Girls,Songea Boys,Londoni,Msamala na Emanuel Nchimbi.
Serikali kupitia TAMISEMI imetenga shilingi bilioni 29 katika Halmashauri zote nchini ili kujenga miundombinu ya shule yakiwemo madarasa 478 na mabweni 269 ili kuhakikisha wanafunzi wote waliokosa nafasi ya kupangiwa kidato cha tano,wanapata katika awamu ya pili.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina shule za sekondari za serikali 40 kati ya hizo sekondari za serikali ni 24 na sekondari zisizo za serikali 16.
Kwa upande wake Afisa Taaluma sekondari wa Manispaa hiyo Mkinga Mkinga amesema manispaa hiyo inaendelea kufanya maandalizi ya mitihani ya MOCK mkoa ambayo inatarajia kufanyika kuanzia Julai 9 hadi 21 mwaka huu.
“Lengo la maandalizi ya mitihani hii ni kuhakikisha tunaweka ushindani kwa maandalizi mazuri ya wanafunzi kitaaluma ili kufikia malengo ya mkoa ya kuinua ufaulu toka asilimia 85 na zaidi ya asilimia 90’’,anasisitiza Mkinga.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 23,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa